Imeelezwa kuwa katika kipindi cha mavuno, matukio ya ubakaji kwa wanawake na wasichana hujitokeza zaidi mkoani Morogoro, huku chanzo kikielezwa kuwa ni uwepo wa ngoma za kienyeji zinazochochea ulevi uliokithiri hivyo wanaume wengi kuingiwa na tamaa za kimwili.
Hayo yamebainishwa na na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, SACP Wilbroad Mutafungwa, kufuatia uwepo wa matukio mbalimbali ya ubakaji mkoani humo.
''Katika kipindi hiki cha mavuno, matukio ya ubakaji kwa kiasi kikubwa yanajitokeza sana hasa kwenye sherehe za ngoma na kumtoa binti, na ngoma za kienyeji zinazopelekea watu kulewa pombe na kujikuta kina mama na wasichana wakibakwa''.
Aidha amesema Jeshi la Polisi mkoani humo linaendelea na jitihada za kuwaelimisha wananchi kuachana na masuala ya namna hiyo.
''Nitoe wito, sherehe za namna hiyo kimsingi hatuzikatazi lakini zifuate utaratibu uliowekwa kwenye serikali za mitaa na vijiji, zipate vibali ili kuepuka watu kufanya ulevi uliopitiliza na hatimae kuingiwa na tamaa za kimwili''.