Mfanyabiashara wa Kenya Raphael Ongangi aliyetekwa nyara nchini Tanzania kutokana na madai ya kisiasa amepatikana mjini Mombasa.
Raphael Ongangi alitekwa Jumatatu usiku katika viunga vya mitaa ya Oysterbay jijini Dar es Salaam na watu wenye silaha akiwa na mke wake Veronica Kundya.
Mkewe Veronica amethibitisha kupatikana kwa mumewe mapema leo siku ya Jumanne.
''Nimezungumza naye mwenyewe yupo Momabasa , tumezungumza kwa ufupi anashukuru sana'', ameliambia gazeti la Mwananchi.
Kwa mujibu, wa taarifa zilizoripotiwa na vyombo vya habari nchini Kenya na Tanzania, watu wasiojulikana waliwafuatilia wanandoa hao na kisha kulizuia gari yao na kumchukua bwana huyo na kuondoka naye.
Awali bi Veronica anasema aliamriwa na watu hao ambao anadai walijatambulisha kama maafisa wa usalama kuwa asiseme chochote mpaka atakapotaarifiwa nao.
Na baada ya takribani saa moja akapokea simu kutoka kwa mumewe iliyomtaka kurejea nyumbani na wala asiripoti tukio hilo mahali popote.
Taarifa zilichapishwa kwenye mitandao ya kijamii zinaripoti kuwa Ongangi aliingia Tanzania mwanzoni mwa miaka ya 2000 kwa masomo ya elimu ya juu katika moja ya vyuo vikuu nchini humo.
Udukuzi wa mitandao ya Zitto kabwe
#Baada ya masomo alibaki nchini humo na kuanza biashara na inaripotiwa kuwa ana miliki na kuendesha biashara ya kusafirisha mizigo kutoka bandari ya Dar es Salaam kwenda Rwanda, Zambia na Jamuhuri ya Kidemokrasi ya Congo (DRC).
Tukio la Ongangi kutekwa lilichukua sura mpya baada ya Kiongozi wa chama cha upinzani cha ACT-Wazalendo Zitto Kabwe kuhusianisha kushikiliwa kwake mateka na kudukuliwa kwa mitandao yake ya kijamii.
Ongangi na Zitto wana usuhuba, na mfanyabiashara huyo ameshawahi kuwa msaidizi wa Kabwe.
Zitto aliwaambia waandishi jijini Dodoma wiki iliyopita kuwa waliomteka Ongangi walidukua mitandao yake ya kijamii.