BARUA YA MAJIBU YA AWALI.
Ndugu Abdulrahman Kinana, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu; Ndugu Yussuf Makamba, Katibu Mkuu wa CCM Mstaafu; DAR ES SALAAM.
Tarehe15 Julai, 2019.
Nakiri kupokea barua yenu ya tarehe 15 07/ 2019 ambayo mliisaini wote wawili, na ikawasilishwa kwangu kwa mkono na Mhe. Nape Nnauye (Mb), jana tarehe 14/07/ 2019.
Baada ya kuisoma kwa makini, nimetambua kwamba malengo makuu ya barua hiyo, yalikuwa ni mawili yafuatayo:
(i) Kuwasilisha kwa pamoja malalamiko yenu dhidi ya mtu aitwaye Cypriian Musiba; ambaye “amekuwa akitoa maelezo yenye kuwatuhumu na kuwazushia uwongo ninyi, na viongozi wengine wastaafu wa CCM na wa Serikali waliostaafu na walioko madarakani, kwamba eti mnamhujumu Rais kutekeleza majukumu yake” (ukurasa wa kwanza, para ya pili).
(ii) Kuomba Baraza la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM “walishughulikie jambo hili, kwa namna ambayo wazee wenyewe wataona kuwa inafaa”. (ukurasa wa pili, para ya mwisho).
Zaidi ya hayo, nimezingatia maelezo yenu ya kuwa “tuliamini kwamba, kama utaratibu wa CCM ulivyo, kazi ya kulinda heshima ya CCM ni pamoja na kukemea vikali, pale viongozi wake wakuu wa sasa na waliostaafu wanapochafuliwa. Kwa hiyo basi, tulitegemea wahusika ndani ya Chama watazikemea kauli zake , na kumuasa asitumie jina la Mwenyekiti wa CCM kuchafua na kudhalilisha watu, au kumchukulia hatua nyingine muafaka. Kwa bahati mbaya, hili halikufanyika”. (ukurasa wa kwanza, para ya tatu).
Kwa maelezo hayo, barua yenu inachukua sura ya “rufaa kwa Wazee” hawa, kutokana na kuona kwamba Chama “kimeshindwa kukemea vikali jambo hili”.
Majibu ya awali.
Kama mnavyofahamu, Baraza hili hufanya kazi kwa njia ya vikao rasmi, na kwamba Katibu peke yake hana mamlaka ya kutoa maamuzi yoyote. Kwa hiyo, nitawasilisha barua yenu kwa Wajumbe wa Baraza, ili kupata maelekezo yao juu ya nini kifanyike. Lakini wakati tunasubiri, naweza kutoa majibu ya awali, yakiwa ni ya kukumbushana mambo ya msingi yafuatayo ambayo yanapaswa kuzingatiwa, (ambayo mimi na ninyi tulisimamia utekelezaji wake, wakati tulipokuwa madarakani kama viongozi wakuu wa Chama):
(1) Wajibu wa kutii Katiba na Kanuni zilizopo.
Jambo la kwanza linahusu mamlaka ya kutenda kazi, au ‘ jurisdiction’, ya Baraza letu, kama yalivyowekwa na Katiba ya Chama, Kama mnavyojua, Katiba ya Chama cha Mapinduzi imekipangia kila Kikao cha Chama kazi zake mahsusi za kufanya. Na kazi mahsusi ya Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, zimetajwa na kuainiishwa katika Ibara ya 127 (3) ya Katiba hiyo, Toleo la 2012, kuwa ni “kutoa ushauri kwa Chama cha Mapinduzi, na kwa Serikali zinazoongozwa na Chama hicho”. Lakini kazi zile za kuangalia mwenendo wa wanachama na Viongozi wake, na kuchukua hatua stahiki pale inapobidi; hizo zimepangiwa vikao vingine vya Chama, vikao ambavyo ni vya utendaji (administration) ; kama ilivyoainishwa katika Ibara zinazohusu Vikao hivyo. Maana yake ni kwamba Kikatiba, Baraza la Ushauri halikupewa mamlaka, au ‘jurisdiction’, ya kutenda kazi hizo, ambazo ni za ki-uendeshaji. Badala yake, jukumu hilo limetolewa kwa vikao vingine, ambavyo ni vya viongozi walioko madarakani.
(2) Jambo la pili linahusu umuhimu wa kuzingatia miiko ya utoaji ushauri (ambayo ndiyo kazi mahsusi ya Baraza hili); ambayo ni hii ifuatayo:
(i) Kwamba ushauri huombwa. Ushauri kamwe hauwezi kushinikizwa kwa mshauriwa, au kutolewa kwake
kama amri ! Ndiyo kusema kwamba ushauri hauwezi kutolewa pale ambapo hauhitajiki. Na mwenye kuamua kuwapo kwa hitaji hilo, ni yule anayehitaji kupata ushauri, SIYO yule anayetaka kutoa ushauri.
(ii) Hata pale ushauri unapotolewa, tusisahau kwamba unaweza ama kukubaliwa; au kukataliwa. Pale unapokubaliwa, thamani yake inakuwa ni kubwa, kwa maana ya kuondoa tatizo lililokuwapo. Lakini pale ushauri unapokataliwa, thamani yake inakuwa ni sifuri kabisa, kwa maana ya kutatua tatizo lililopo.
(3) Jambo la tatu, ni kwamba jukumu la mtu yeyote aliyetuhumiwa la kusafisha jina lake, ni la mtuhumiwa mwenyewe.
Barua yenu imeeleza kwamba “Mlitafakari suala la kujitokeza hadharani ili kutoa yaliyo moyoni mwenu katika kujibu uwongo wake, kusafisha majina yetu, heshima yenu, na rekodi nzuri ya utumishi wenu, lakini mkaona kuwa ni vyema kwanza mkawasilisha malalamiko yenu kwenye Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, ili jambo hili lishughulikiwe”.
Sasa ki-utaratibu, siyo sahihi kujaribu kukwepa jukumu hilo la watuhumiwa wenyewe kujisafisha kwa kukanusha tuhuma zinzowahusu, na kujaribu kulihamishia jukumu hilo kwa watu wengine . Hii ni kwa sababu watuhumiwa wenyewe ndio wanaojua ukweli kuhusu tuhuma hizo, na kama kweli hazina msingi, ni wajibu wao kufichua ukweli wanaoujua.
Umuhimu wa jambo ili unatokana na kuwapo kwa dhana inayosema kwamba “silence means consent”; ambayo maana yake ni kwamba ‘ukinyamaza kimya bila kukanusha tuhuma zilizoelekezwa kwako, ukimya wako huo unachukuliwa kwamba umekiri ukweli wa tuhuma hizo’. Nafurahi, na kuwapongeza, kwamba tayari mumetekeleza wajibu huo kupitia vyombo vya habari.
TAHADHARI: Msiruhusu machungu ya tuhuma hizo yakawasahaulisha misingi hii, mkashawisika ‘kutafuta njia za mkato’ za kuyashughulikia, ambazo kumbe zinakiuka Katiba ya Chama chetu.
Madhumuni ya maelezo haya
Naomba ieleweke kwamba madhumuni ya kukumbushana juu ya mambo haya ya msingi , ni kuonesha tu ugumu uliopo wa ki-Katiba, kwa Baraza la Ushauri la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM kushughulikia malalamiko yenu, kama mlivyoomba. Ugumu huo unatokana na kuzingatia kuwa:
kwanza, Katiba ya Chama haikutoa jukumu la kufanya kazi za ki-uendeshaji (administration) kama hii ya kusikiliza malalamiko yenu, kwa Baraza hili. Lakini pili, Baraza letu pia halikupewa mamlaka ya kusikiliza rufani zinazotolewa dhidi ya Chama, kama hii ya kwenu.
Ni muhimu vile vile, kuzingatia kwamba Baraza la Viongozi Wakuu Wastaafu wa CCM, ni chombo maalum cha Chama hicho , kilichoundwa na kupewa kazi maalum, iliyotajwa katika Katiba ya Chama. Baraza hili siyo kundi lolote tu la “wazee wa Chama” (kama yalivyo yale “Mabaraza ya wazee” mengine, yaliyotajwa katika Ibara ya 128 ya Katiba ya Chama), ambayo wajumbe wake wanatajwa kuwa ni “wazee wote wana-CCM, wenye umri kuanzia miaka sitini”; ambao, kwa kuwa hawakupangiwa jukumu lolote maalum, wanadhaniwa kuwa wanaweza kushiriki tu katika utekelezaji wa shughuli zozote za Chama “kwa kutumia busara za uzee wao, kama watakavyoona wao kuwa inafaa”!
Nahitimisha kwa kurudia kusema, kwamba haya ni majibu ya wali tu. Nawajibika kusubiri maelekezo ya wajumbe wa Baraza.
Pius Msekwa.
KATIBU, BARAZA LA USHAURI LA VIONGOZI WAKUU WASTAAFU WA CCM.