Mwandishi wa Habari mikononi mwa TAKUKURU kwa kuomba rushwa


Na John Walter-Manyara

Taasisi ya kuzuia na kupambana na Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Manyara inamshikilia Patrick Michael Chambo mwandishi wa habari wa kujitegemea kwa tuhuma za kuomba Rushwa ya shilingi laki tatu kwenye kiwanda cha Pombe kali Cha Mati Super Brand Ltd mjini Babati.

Inaelezwa kuwa Mtu huyo  aliomba rushwa hiyo kwa kuwatisha wamiliki wa kiwanda hicho kuwa anayo taarifa zinazohusu kiwanda hicho kukwepa kulipa kodi ya serikali hivyo angewaandika vibaya asipopewa kiasi hicho cha pesa.

Mkuu wa Takukuru mkoa wa Manyara Fidelis Kalungura ameiambia Muungwana Blog  kuwa mtuhumiwa huyo aliendelea kufanya mawasiliano kwa njia ya simu na mmoja wa wakurugenzi wa Mati Super Brand Ltd ambapo ilipofika tarehe 2 April mwaka huu alipokea hongo ya shilingi 150,000 kwa  njia ya Mpesa ikiwa ni sehemu ya fedha alizoziomba ili asiziandike taarifa hizo kwenye vyombo anavyo viandikia.

Kwa kuwa TAKUKURU waliendelea kumfuatilia mtu huyo,walifanikiwa kumkamata wilayani Korogwe mkoani Tanga June 28 na kusafirishwa hadi Babati  ambapo baada ya kuhojiwa  alipata dhamana na kutakiwa kurudi July 9 lakini alikiuka masharti ya dhamana hadi alipokamatwa tena July 19 wilayani Hai mkoa wa Kilimanjaro.

Hata hivyo Kalungura ameeleza kuwa mtuhumiwa huyo anashikiliwa na TAKUKURU mkoani hapa na anatarajiwa kupandishwa mahakamani muda wowote taratibu za kisheria zitakapokamilika ili kujibu tuhuma hizo.

Kalungura amewataka waandishi wa habari na wananchi wote wa mkoa wa Manyara wajiepushe na vitendo vya rushwa na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria,kanuni na taratibu pamoja na maadili ya kazi zao,vinginevyo watakumbana na mkono wa Sheria.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad