Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli amempokea mgeni wake Rais wa Jamhuri ya Kenya, Uhuru Muigai Kenyatta amewasili katika uwanja wa ndege wa Chato Mkoani Geita.
Katika hotuba yake, Rais Magufuli amesisitiza ushirikiano wa nchi hizo mbili kwani ndio kichocheo kikubwa cha biashara, huku akikemea kauli zenye kuleta mgawanyiko.
"Biashara kati ya Tanzania na Kenya 2018 ilikuwa ya Tril. 1, Tanzania iliuza bidhaa zenye thamani ya Bil. 400 na kuagiza bidhaa za Bil 500, kwa mujibu wa TIC Kenya ni miongoni mwa nchi 5 zinazowekeza Tanzania, kuna miradi 504" alisema Rais Magufuli.
Ameendelea kwa kusema, "Nikupongze Rais Kenyatta na Serikali yako kwa hatua mlizochukua, dhidi ya mtu aliyetoa kauli ya kuwagawa Watanzania na Wakenya, maneno ni sumu kali sana nakuthibitishia sisi Watanzania tunawapenda sana Wakenya,".
Hapo awali Rais Kenyatta naye alisema, "Kuna watu wanaropoka huko, unawezaje kuzuia Mtanzania asifanye biashara Kenya au Mkenya asifanye Biashara Tanzania. Tunataka kushirikiana na kuona ushirikiano unakua na ndio maana tumeona sio kila siku ziara za Kitaifa, leo nataka nikale Sato kwake".