Lugola ameyasema hayo leo, katika Kata ya Butimba, jimboni kwake, alipokuwa anazungumza na wananchi wa Kijiji cha Mwiseni, mara baada ya kushiriki shughuli za mazishi ya mtoto wa dada yake katika Kijiji hicho, aliyefariki hivi wiki hii mkoani Mwanza.
Lugola alisema Tanzania ina amani kwasababu inautamaduni wa kuwa na amani, hivyo asitokee mtu akaharibu utamaduni huo ambao nchi inaendelea kuhudumisha.
“Ndugu zangu wana Mwiseni, Wana Mwibara, amani tulionalo ndiyo inatuwezesha leo tunalima vizuri, tunavua samaki, leo tunakula vizuri, leo tunafanya shughuli mbalimbali za maendeleo, hivyo tuendelee kuitunza amani hii,” alisema Lugola.
Aliongeza kuwa, Wizara yake kupitia Jeshi la Polisi ipo imara, Serikali ya Rais Dkt. John Magufuli ipo imara na inaendelea kuwalinda Watanzania mahali popote walipo nchini, na hakuna mtu atakaye ivunja amani hiyo.
Aidha, Lugola aliwataka wananchi hao kuhifadhi vyakula vizuri ili kuepusha janga la njaa kwa hapo baadaye na kusababisha wananchi kuja kuteseka kwa ukosefu wa vyakula na kusababisha mateso katika familia.
“Tutunzeni vyakula vyetu, msitumie hovyo, kuweni makini na matumizi ya vyakula, sitaki nije kuona mnateseka na njaa, hakikisheni mnatunza vyakula kwa ajili ya matumizi ya baadaye, ogopeni njaa kama ukoma,” alisema Lugola.
Lugola ambaye pia ni Mbunge wa Jimbo hilo, alifanya ukaguzi wa miradi ya maendeleo akikagua madarasa ya shule ya msingi pamoja na zahanati.
“Nataka hili darasa likamilike kwa wakati, natoa mifuko ya saruji 100 ili kuikalimisha zahanati hii katika Kata hii, na pia nitaleta mabati ili maendeleo yazidi kuwafikia wananchi wa jimbo hili,” alisema Lugola.
Waziri Lugola ameanza ziara yake leo, ambapo anatarajia kufanya ziara hiyo katika vijiji vya Kata zote jimboni humo.