Jeshi la Polisi limejipanga vizuri katika ulinzi kipindi cha Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Nchi za Kusini mwa Afrika (SADC) ambao utahudhuriwa na wakuu wa nchi 16 Afrika.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, msemaji wa jeshi hilo, alisema kuwa jeshi hilo limejiandaa kikamilifu kwa ajili ya ulinzi kwa siku za mkutano huo. Alisema jeshi limejiandaa kikamilifu kuhakikisha ulinzi na usalama unaimarishwa kuanzia ugeni utakapoingia nchini mpaka utakapomaliza mkutano na kuondoka.
"Katika mkutano huo, shughuli mbalimbali zitakuwa zikiendelea kama vile wiki ya viwanda, mikutano ya awali pamoja na mkutano wenyewe wa wakuu wa nchi na serikali, jeshi la polisi limejipanga vizuri kwa ulinzi,"alisema.
Alisema ulinzi huo ni katika kuhakikisha na kutekeleza majukumu yake ya kulinda maisha ya raia na mali zao pamoja na wageni wote watakaofika nchini. Misime alisema jeshi hilo pia linatoa wito kwa wananchi kuendelea kutii sheria za nchi ikiwemo sheria za usalama barabarani na pia kutoa taarifa kwenye kituo cha polisi wanapotia shaka katika jambo lolote.
Wakati huo huo, jeshi hilo limetoa taarifa ya ajali ya gari iliyoua askari wake watatu Julai 25 mwaka huu katika eneo la kijiji cha Kilimahewa barabara ya Kilwa wilaya ya Mkuranga.
Kamanda Misime aliwataja askari waliopoteza maisha katika ajali hiyo kuwa ni Ofisa Mnadhimu Mkoa wa Kipolisi Rufiji, Kamishna Msaidizi wa Polisi, Issah Bukuku, Inspekta Asteria wa ofisi ya Mkuu wa upelelezi Rifiji na askari namba G1132 Pc Lameck wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU).