Akizungumza na EA Radio, Prof. Mkumbo amesema kuwa kwa sasa anatekeleza majukumu aliyokabidhiwa na Rais Magufuli kuhakikisha kuwa maji yanatoka maeneo mbalimbali nchini na ikifika wakati husika ataamua endapo atagombea ama vinginevyo.
"Suala la Ubunge kwa sasa bado, ninachapa kwanza kazi aliyonikabidhi Rais Magufuli. Imebaki miezi 12 ya kujua hatma na maamuzi ya endapo nitagombea ama vinginevyo", amesema Prof. Mkumbo.
Pia amezungumzia juu ya kero sugu za maji zinazosumbua maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es salaam kama Gongo la mboto, Chanika, Goba na maeneo mengine ambayo miradi haijakamilika, ambapo amesema mchakato wa kukamilisha miradi hiyo unakwenda kwa kasi na ndani ya miezi 12 ijayo wananchi wataanza kutumia maji.
"Wananchi wa Dar es salaam na maeneo mengine nchini wasiwe na wasiwasi, serikali inaendelea kutekeleza ilani ya CCM kwa ufanisi, mpaka kufikia April mwaka huu tumeweza kuwasambazia maji wanannchi kwa asilimia 65 na malengo yetu mpaka mwisho wa 2020/21 tutakuwa tumewafikia wananchi kwa asilimia 85", ameongeza.
Profesa Kitila Mkumbo alikuwa mshauri wa Chama cha ACT-wazalendo kabla ya kuteuliwa na Rais Magufuli, April 04, 2017 kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji ambayo bado anahudumu mpaka sasa