Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF) na Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) wamewasogezea karibu huduma Wanachama wa Mifuko hiyo katika msimu huu wa Maonesho ya 43 ya Bishara ya Kimataifa ya Dar es Salaam maarufu Sabasaba.
Wakizungumza Julai 2, 2019 kwa nyakati tofauti Wakurugenzi Wakuu wa Mifuko hiyo, Bw. Hoseah E. Kashimba (PSSSF) na Bw. William Erio (NSSF) wamesema kuwa wameamua kufanya maonesho hayo kwa kushrikiana ili kuwarahisishia Wanachama kupata huduma wanazohitaji wote wakiwa kwenye banda namba 13 lililo mkabala na jingo la matangazo ndani ya viwanja vya Sabasaba.
“Tukiwa katika banda hili kwa kushirikiana na wenzetu wa NSSF ambao wao wanashughulika na wafanyakazi kutoka Sekta Binafsi na sisi PSSSF tunahudumia wafanyakazi kutoka Sekta ya Umma.”
Tumeona tufanye maonesho haya pamoja kwa sababu ya kutoa elimu kwa wanachama kwa urahisi zaidi hasa kwa vile hatuko katika ushindani kama ilivyokuwa hapo awali, hii itasaidia kama Mwanachama anataka kujua taarifa kuhusu Mafao yake kama anatoka Sekta binafsi ataelekezwa aende NSSF na kama anatoka Sekta ya Umma ataelekezwa aende PSSSF, amefafanua Bw. Kashimba.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkuu wa NSSF Bw. William Erio alisema “Baada ya kuunganishwa Mifuko hapo mwaka jana bado watu hawajaelewa vema tofauti zilizopo kwa hiyo wanakuja hapa kama banda pekee linalotoa huduma ya Hifadhi ya Jamii na wakifika basi wanaelekezwa katika sehemu husika na kupata huduma wanayohitaji.” Alisisitiza Bw. Erio.
Alisema ni sehemu ambayo watu wanaweza kuja na kujibiwa maswali yote waliyonayo na kutatuliwa kero zao.
Maonesho hayo ya kila mwaka yamefunhguliwa rasmi Julai 2, 2019 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na yanatarajiwa kufikia kilele Julai 13, 2019.