Rais Magufuli kuweka jiwe la msingi mradi wa Stiegler’s Gorge

Rais wa Tanzania, Dk. John Magufuli kesho anatarajiwa kuweka jiwe la msingi mradi wa kuzalisha umeme wa maji maporomoko ya Mto Rufiji (Stiegler’s Gorge) ambao ujenzi wake utakamilika ndani ya miezi 35.

Mradi huo ambao ujenzi wake umefika asilimia 15, hadi kukamilika utagharimu Sh trilioni 6.5.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu mradi huo mjini Morogoro, Waziri wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, alisema kukamilika kwake kutaweka historia nyingine kwa nchi na usimamizi unaofanywa na Rais Dk. Magufuli.

Alisema mradi huo wa kufua umeme wa megawati 2,115 kwa kutumia maji, unaendelea kutekelezwa na sasa uko tayari kuwekwa jiwe la msingi.

“Kwa hatua za usimamizi wa mradi hadi sasa tupo asilimia 100, ila katika hatua za utekelezaji wake tupo asilimia 15 hadi sasa.

“Mkandarasi alikuwa na kazi ya kukabidhiwa maandalizi ya mradi na kazi ambayo anaendelea nayo ni kuchoronga eneo la bwawa na ujenzi wa madaraja.

“Kukamilika kwa mradi kutaliwezesha taifa kuwa na umeme wa kutosha na wa uhakika, unaotabirika na wa gharama nafuu kwa watumiaji,” alisema Dk. Kalemani.

Alisema mradi huo utawezesha nchi kufikia uchumi wa viwanda na kuimarisha shughuli za kiuchumi na kijamii kwa kuendeleza kilimo cha umwagiliaji, uvuvi, kukuza utalii na kuongeza ajira kwa Watanzania.

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad