Tundu Lissu: Nina Haki ya Kugombea Urais Nitapoteza sifa kama nitakutwa na hatia na Mahakama au Sekretarieti ya maadili
0
July 02, 2019
Aliyekuwa mnadhimu wa kambi ya upinzani bungeni nchini Tanzania, Tundu Lissu amesema licha ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kudai hakujaza fomu za mali na madeni za viongozi wa Umma bado ana sifa za kugombea nafasi yoyote ya uongozi.
Lissu aliyeko Ubelgiji kwa matibabu amenukuliwa na gazeti la Mwananchi ikiwa ni siku chache zimepita tangu alipopoteza sifa za kuwa mbunge.
"Ili upoteze sifa ya kugombea ubunge au urais sharti uwe na hatia, sasa mimi sijakutwa na hatia na mahakama au mahakama ya Sekretarieti ya maadili, Ndugai peke yake hawezi kunitia hatiani bila kunisikiliza."
"Kwa hiyo mimi naweza kugombea nafasi yoyote ya uongozi iwe ubunge au urais. Kama wanataka nisigombee wanipeleke mahakamani au kwenye mahakama ya sekretarieti na wakiniuliza kwa nini sijajaza fomu nitawaambia nitawezaje kujaza nikiwa nje ya nchi," amesema Lissu
Amesema fomu hizo zinapaswa kujazwa na kuziwasilisha kwa njia ya mkono lakini zinapaswa kusainiwa na wakili wa Tanzania, "Sasa mimi niko hospitalini Ubelgiji, nawezaje kuzijaza, huku nampata wapi wakili, nawezaje kuzipeleka kwa mkono? Kwa hiyo walipaswa kuniuliza kwa nini sijajaza na si kuzungumza sijajaza bila kuwa na sababu."
Mvutano ulianzia wapi?
Spika wa Bunge la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Job Ndugai alitaja sababu kuu mbili zilizomsukuma kuiandikia tume ya uchaguzi, mosi ni kutokana na Lissu kutokuhudhuria bungeni kwa muda mrefu na pili kutokuwasilisha fomu ya tamko la mali na madeni kwa sekretari ya maadili kwa mujibu wa sheria.
Lakini Lissu amezipinga hoja zote mbili, akisema hashangazwi na tamko la Spika Ndugai.
Tags