UCHOKOZI WA EDO: Akina Jaguar Wapo Wengi Duniani Kwa Sasa
0
July 02, 2019
By Edo Kumwembe
Wiki iliyopita kulizuka kasheshe kidogo wakati mbunge mmoja wa pale Kenya, Mheshimiwa Jaguar alipotaka wafanyabiashara wa kigeni, hasa Watanzania waondoke nchini humo. Nilitabasamu. Mfano mwingine umejitokeza.
Mashariki, Magharibi, Kusini na Kaskazini, dunia imeanza kupata watu wenye akili tofauti. Huyu Jaguar sio mwehu. Ana akili timamu. Ana akili nyingi. Katika dunia ya leo viongozi wengi huwa wanatumia. Ni akili ambayo zamani aliitumia marehemu Christopher Mtikila.
Unakusanya watu na kuwaaminisha kwamba matatizo yao yanatokana na wageni au wahamiaji. Ukifanya hivi unamaliza kazi kirahisi. Unaweza kuanza kuhesabika kuwa shujaa wa ghafla. Tumezalisha viongozi ambao kila mmoja kwa nafasi yake ana uwezo wa kuwatumia watu wa eneo lake kwa kauli hii.
Hata Donald Trump alipanda chati kwa Wamarekani baada ya kuanza kupiga mikwara ya ukuta dhidi ya Wamexico. Akapiga mkwara wa kuwarudisha kwao watu weusi, wazamiaji. Akapiga mkwara wa kuwanyima viza watu weusi. Akapanda chati kwa wazawa.
Akina Julius Malema pale ‘Bondeni’ Afrika Kusini, nao wanakuwa na mikakati kama hii kwa ajili ya kujiongezea umaarufu wa kisiasa. Sio kwamba hawajui wnaachokifanya, hapana, wanajua lakini wanajificha katika bustani ya mchicha.
Hata sisi tuna matatizo yetu kibao ya kiutawala ambayo yamesababisha tuendelee kuwa maskini. Ni matatizo ‘yetu’ zaidi kuliko kudai ni ya wengine lakini tunajidai kwamba mabeberu ndio tatizo letu la msingi. Ni namna tu ya kuhamisha mpira uende eneo jingine.
Majuzi Waingereza nao wakajiingiza katika mkumbo wa Brexit (kujitoa Jumuiya ya Ulaya). Wakataka kujitenga na wenzao. Ilikuwa namna moja tu ya kuonyesha kwamba matatizo yao yanatokana na wengine. Nasikia wamekwama. Sisi tulioishia darasa la saba tulishangaa kasi yao ya kujitoa, kama tunavyoshangaa namna walivyokwama.
Kukwama kwao ni kama ambavyo Jaguar atakwama au watu wenye mawazo yake watakavyokwama. Tatizo ni kwamba hapo katikati dunia iliruhusu sana kusaidiana. Kwa sasa kuishi kwa kujitegemea ni ngumu hata kama una utajiri usiomithimilika.
Jaguar anajua ni kwa kiasi gani kuna Wakenya wengi nje ya nchi yake kuliko Waganda au Watanzania waliopo nje ya nchi zao. Hata hivyo, analazimika tu kujitoa ufahamu kwa muda ili kujiongezea umaarufu.
Mwananchi
Tags