UCHOKOZI WA EDO: Wengi Tungetamani Kuwa Faru Rajabu Lakini Tatizo...


Edo  Kumwembe

Juzi Namba Moja akatuomba wananchi wake tuwe kama Faru Rajabu. Ni yule faru aliyefanya maajabu ya kuzalisha wenzake wengi kuanzia mwaka 2016 mpaka leo. Namba Moja alikuwa anatukumbusha kwamba idadi ya watu itasaidia katika maendeleo yetu.

Inawezekana alikuwa sahihi kwa mfano wa nchi ya China. Ni kweli wengi tungependa kuwa kama Faru Rajabu, tatizo linakuja wakati wa kulipa ada na kupeleka watoto hospitali. Hapo ndipo unapogundua kwamba ‘ukidume’ wako hauna maana mbele ya kadi zako za benki.

Unajaribu kupima ubora wa elimu yetu ya kawaida, unagundua kwamba ili watoto wako washindane lazima wakasome shule zile wanazofundishwa ‘viingereza’ kwa ajili ya kupambana na maisha siku za usoni. Ikifika Januari na Julai ndipo unapogundua haina maana ya kuwa Faru Rajabu. Ada zinaumiza.

Kama hiyo haitoshi pata safari ya kwenda vijijini. Machozi yanaweza kukutiririka kutokana na picha utakayoipata huko na kukufanya uamini kwamba mtoto wa kijijini daima ataendelea kutawaliwa na mtoto wa mjini pindi zitakapofika zama zao za utu uzima. Mtoto wa kijijini hawezi kupambana tena kwa sababu bado ana elimu ya ‘Kayumba Primary School’. Vipi kama baba yake akijifanya Faru Rajabu zaidi?

Elimu ya ‘Kayumba Primary School’ haiwezi kumfanya alikomboe Taifa. Elimu ya kukariri. Elimu ya jembe la mkono. Hata tukijazana itatusaidia nini? Nadhani tujikite kwanza katika maendeleo ya viwanda, kilimo na teknolojia kabla ya kurithi nyayo za Faru Rajabu.

Kwa sasa tujifunze kuachana na maamuzi mengi ya kisiasa na tujikite katika uzalendo halisi wa kuikomboa nchi kiuchumi kuliko kisiasa. Tukivuka malengo kidogo tu nadhani tunaweza kuiga nyayo za Faru Rajabu.

Mwananchi

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad