Ufafanuzi Kuhusu Taarifa Zilizoandikwa Kwenye Magazeti Na Mitandao Ya Kijamii Kuhusu Uwepo Wa Dawa Mpya Ya Asili Inayotibu Saratani Ya Tezi Dume
0
July 15, 2019
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu (NIMR) ilianzishwa kwa sheria ya Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Namba 23 ya mwaka 1979. NIMR ni taasisi chini ya Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto. Taasisi hii pamoja na kufanya utafiti, inaratibu, inakuza na kusimamia tafiti za afya zinazofanyika nchini na kukuza matumizi ya matokeo ya tafiti hizo.
NIMR ina idara ya tafiti za tiba asili ambayo jukumu lake ni kufanya utafiti juu ya dawa za miti-shamba, ambazo nyingine zimekuwa zinatumika miaka mingi na bibi na babu zetu. Idara ya tafiti ya dawa asilia mwaka huu iliiwakilisha NIMR kwenye maonesho ya Sabasaba katika banda la Tume ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH).
Lengo la kushiriki katika maonesho haya ni kuonesha ubunifu katika tafiti za afya zinazofanyika NIMR. Waandishi wa habari walimhoji mtafiti wa NIMR katika banda la COSTECH na wameripoti kwamba NIMR imegundua dawa ya kutibu saratani ya tezi dume. Kutokana na uzito wa suala hili na kuzingatia mateso ya wagonjwa wenye tezi dume NIMR ingependa kufafanua na kurekebisha taarifa zilizotolewa na vyombo vya habari na kusambaa katika mitandao ya kijamii.
Ni kweli kwamba moja ya dawa za miti-shamba ambazo NIMR imetengeneza imeonesha dalili ya kupunguza uvimbe kwa wagonjwa wenye tatizo la kuvimba tezi dume. Dawa hii haijaonesha uwezo wa kutibu saratani ya tezi dume. Dawa hii bado iko katika hatua ya uchunguzi wa kitafiti. Lengo letu la kushiriki katika maonesho ya Sabasaba lilikuwa ni kuonesha ubunifu katika tafiti za afya.
Baadaye kama tafiti hizo zitakuwa na matokeo mazuri zinaweza kutumika baada ya kufuata hatua za kisheria za usajili. Tunaomba radhi kwa wale wote walioathirika kwa namna moja au nyingine na ripoti hiyo iliyokuwa inasambaa.
Taarifa imetolewa na:
Mkurugenzi Mkuu
Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu
3 Barabara ya Barack Obama
S.L.P. 9653, Dar es Salaam
Simu: +255 22 2121400; Barua pepe: dg_office@nimr.or.tz
Tags