Rais wa Kenya, Uhuru Kenyatta amemtumia ujumbe maalumu Rais wa Tanzania, Dkt. John Magufuli unaoelezea msimamo wa Serikali yake kuhusu kukerwa na matamshi yaliyotolewa hivi karibuni na Mbunge wa jimbo la Starehe, Charles Njagua Kanyi maarufu kwa jina la Jaguar.
Ujumbe huo wa maandishi umewasilishwa na Balozi wa Kenya nchini, Dany Kazungu na kupokelewa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa niaba ya Rais Dkt. Magufuli, ofisini kwa Waziri Mkuu Magogoni jijini Dar Es Salaam.
Akipokea taarifa hiyo Waziri Mkuu amesema Watanzania wamefurahishwa na hatua mbalimbali zilizochukulia na Serikali ya Kenya dhidi ya mbunge huyo zinazodhihirisha kwamba matamshi hayo hayakuwa msimamo wa Serikali ya Kenya wala wananchi wake bali ulikuwa ni msimamo binafsi wa mbunge huyo.
"Uhusiano kati ya Kenya na Tanzania ni wa karibu mno na wa kindugu kwani kuna baadhi ya makabila yapo katika nchi mbili hizi kama vile Wamasai na Wakurya na Wajaluo hivyo ushirikiano katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kabiashara na ya kijamii haukwepeki." amesema Waziri Mkuu
Hivyo, Waziri Mkuu ametoa wito kwa viongozi na wananchi wa nchi za Jumuiya ya Afrika ya Mashariki kujiepusha na kauli zenye viashiria vya kujenga chuki, uhasama na migongano miongoni mwa wananchi kwani kauli hizo zisipodhibitiwa mapema zinaweza kusabisha hofu na kutokuelewana miongoni mwao.
"Mambo yetu yote katika nchi za Afrika ya Mashariki hasa ya biashara na ya kiuchumi kwa ujumla yataenda vizuri endapo tutalinda na kudumisha amani, bila amani tutaogopana na tutashindwa kabisa kushirikiana", amesisitiza Mheshimiwa Majaliwa.
Julai 24, 2019 kupitia mitandao ya kijamii kulisambaa kipande cha video kikimuonesha Mbunge Jaguar, akitoa kauli ambazo zilitafsiriwa zililenga kuleta ubaguzi baina ya wananchi wa Kenya na Tanzania lakini baadaye mwenyewe alikanusha kuwa hakuwalenga watanzania bali walikuwa watu wenye asili ya China.