Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli, ameweka jiwe la msingi la ujenzi wa mradi wa kufua umeme wa Mto Rufiji, utakaogharimu zaidi ya trilioni 6.5, pamoja kuzalisha Megawats za umeme 2115.
Akizungumza katika uwekaji wa jiwe la msingi wilayani Rufiji, Rais Magufuli amesema mradi huo utakuwa na faida kubwa kwa Watanzania hasa kuelekea Tanzania ya viwanda, huku akiwataka Watanzania wasiibe vifaa, wakati wa ujenzi.
"Kwangu mimi ni tukio la kipekee na historia kubwa kwa taifa letu, wazo lilianza 1970 - 1972, Mwl. Nyerere alijua umeme ni kichecheo cha sekta zote, kwa sababu lengo la Serikali ya awamu ya 5 ni kujenga uchumi wa viwanda." amesema Rais Magufuli.
"Nchi yetu imeidhihirishia Dunia, kuwa sisi ni taifa huru linaloweza kujiamulia mambo yake kwa mujibu wa vipengele vyake, mnajua huu mradi ulikumbwa na upinzani mkubwa ndani na nje ya nchi." ameongeza.
Kuhusu suala la ajira kwenye mradi huo, Rais amesema kipaumbele wapewe watu wanaozunguka eneo hilo huku akiwataka watakaopata ajira wasiibe. ''Msiibe vifaa, kuiba ni dhambi na ukiiba umejiibia mwenyewe, naomba vyombo vya ulinzi viuchukue mradi huu kama mboni ya Serikali.
Ujenzi wa mradi huo unatarajiwa kuchukua miezi 42 ambapo kukamilika Juni 22, 2021.