Unaambiwa Mali za MBOWE Zagombaniwa Katika Mnada


Mali za Kampuni ya Mbowe Limited (Bilicanas) vimepigwa mnada leo na Kampuni ya Udalali ya Fosters Auctioneers & General Traders ya jijini Dar es Salaam na kuchangamkiwa na watu waliojitokeza kuzinunua.

Mali hizo ambazo ni za Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema).

Mnada huo umefanyika leo chini ya Joshua Mwaituka, dalali wa mahakama, kwenye ghala la Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) lililopo maeneo ya Bandarini, jijini Dar es Salaam.


Akizungumza kuhusu mnada huo, Mwaituka amesema mwitikio wa wateja umekuwa mzuri, na kwamba asilimia kubwa ya vifaa hivyo vimepata wateja.

“Vitu karibu vyote vimeuzwa, kasoro makochi, bei ni za kawaidia. Mwitiko wa watu ni mzuri wamekuja tangu saa 2 asubuhi, kuna waliondoka lakini hao waliobaki wakasema bora wanunue,” amesema Mwaituka.

Mwaituka ametaja baadhi ya vifaa vilivyopigwa mnada ikiwemo, taa ambazo mteja wa mwisho alifikia bei kiasi cha Sh. 7 milioni, jukwaa (Sh. 5.1 milioni), viti, kreti za bia, genereta, mashine ya kupozea (Cooling System) na samani mbalimbali.

Japhet Mwanasenga, Meneja wa Ukusanyaji Madeni kutoka NHC amesema mnada huo ni muendelezo wa shirika hilo katika kudai deni la zaidi ya Sh. 1 bilioni, kutoka kwa kampuni ya Mbowe Limited (Bilcanas) inayomilikiwa na Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chadema Taifa.

Mwanasenga amesema NHC ilichelewa kupiga mnada mali hizo, kutokana na mmiliki wake (Mbowe) kufungua kesi mahakamani ya kuzuia mali zake kuuzwa.

Aidha, Mwanasenga amesema fedha zitakazopatikana kupitia mnada huo, zitaingizwa katika deni la kampuni hiyo, na kwamba kiasi cha deni kitakachosalia, wahusika watalipa kwa mujibu wa sheria.

“Tulikuwa tunamdai Sh. 1.1 bilioni. Tutatumia taratibu zote zikikamilika tutamjuza kiasi tulichouza, kilichobaki lazima alipe,” amesema Mwanasenga na kuongeza.

“Vitu vilichelewa kuuzwa kwa sababu mbowe alienda kupinga mahakamani kutouziwa vyombo vyake, akashindwa kesi tukauza.”

Vifaa vilivyopigwa mnada ambavyo vilikuwa vinatumika katika klabu ya usiku ya Bilicanas, vilichukuliwa na NHC Mwezi Septemba mwaka 2016, baada ya mmiliki wake kushindwa kulipa deni la zaidi ya Sh. 1 bilioni.

Deni hilo limetokana na malimbikizo ya kodi, ambapo Mbowe kupitia kampuni yake alikuwa mpangaji katika jengo la NHC lililoko makutano ya mitaa ya Mkwepu na Indira Ghandi katikati ya Jiji la Dar es Salaam.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad