UONGOZI wa Simba umesema kuwa, wachezaji wa timu hiyo walianza kutua nchini kuanzia juzi Jumatatu na wanatarajiwa kuingia kambini Julai 15 lakini wataanza kwanza kufanyiwa vipimo hospitalini.
Simba ambayo inatarajiwa kwenda Afrika Kusini kuweka kambi hiyo kwa ajili ya maandalizi ya msimu ujao, mbali na kuwapima afya nyota wake wote, pia itawapa semina maalum na kupatiwa vifaa vyao.
Akizungumza na Championi Jumatano, Mtendaji Mkuu wa Simba, Crescentius Magori, alisema zoezi hilo litafanyika haraka ili kuona linamalizika ndani ya wakati kabla ya kuelekea kambini Afrika Kusini. “Wachezaji Simba walitakiwa kuanza kuripoti kambini tangu juzi kwa ajili ya kufanyiwa vipimo vya afya na kupewa semina maalum.
“Pia kila mmoja atapatiwa vifaa vyake, baada ya hapo ndipo timu itaenda Afrika Kusini kuweka kambi itakayoanza Julai 15, mwaka huu,” alisema Magori.
Magori alisisitiza kuwa wachezaji wa kigeni lazima wafike mapema kwa wale ambao wanaingia Sauz kwa visa. Katika hatua nyingine, chanzo kutoka ndani ya Simba, kimelidokeza Championi kuwa, ndani ya wiki hii, utafanyika usajili wa kutikisa tofauti na hapo awali.
“Kuna usajili wa mchezaji utatikisa wiki hii, mashabiki wetu wajiandae kupata habari njema kuhusu kikosi chao,” kilisema chanzo.
Mpaka sasa, Simba imesajili nyota sita wa kimataifa ambao ni Francis Kahata (Kenya), Tairone Santos da Silva, Gerson Fraga Viera, Wilker Henrique da Silva (Brazil), Sharaf Eldin Shiboub (Sudan) na Deo Kanda (DR Congo).
Huku wazawa ikisajili wanne ambao ni Ibrahim Ajibu, Beno Kakolanya waliotokea Yanga pamoja na Kennedy Juma kutoka Singida United na Miraji Athuman kutoka Lipuli.