Mwanasheria na Wakili wa Kujitegemea, Leonard Manyama amesema kuwa haungi mkono matamshi ya mtu yeyote ya udhalilishaji dhidi ya viongozi wastaafu kwani kufanya hivyo ni kutowatendea haki viongozi hao ambao wamelitumikia taifa kwa mda mrefu.
Ameyasema hayo jijini Dar es salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari ambapo amesema kuwa ni jambo jema kuwaheshimu na kuwaacha wapumzike vizuri na si kuwasumbua.
Amesema kuwa kama kuna mtu anataarifa ya uhalifu wa mtu flani basi kuna utaratibu maalum wa kisheria ambao anapaswa aufuate lakini si kutangaza hadharani kwenye vyombo vya habari na katika mitandao ya kijamii.
Aidha, katika hatua nyingine Manyama amesema kuwa hajafurahishwa na kitendo cha makatibu wakuu wastaafu wa chama cha mapinduzi (CCM), Abdlrahaman Kinana na Yusuf Makamba cha kuandika waraka wa kumlalamkia Cyprian Musiba na kuusambaza kwenye vyombo vya habari kwani badala ya kufanya hivyo walitakiwa wafuate taratibu za kisheria.
”Nimejiuliza maswali mengi sana magumu na majibu yake nimekosa, hawa wazee wetu wastaafu wanajua taratibu zote za kufuata kama wanavyolalamika wamechafuliwa, kwanini wasizifuate? kwanini wasichukue hatua za kisheria? kwanini wakaamua kuandika waraka na kuusambaza kwenye vyombo vya habari wakati taratibu za kufuata wanazielewa, hapa lazima kuna nia ovu dhidi ya serikali,”amesema Manyama
Hata hivyo, Manyama ameongeza kuwa kuna baadhi ya watu ambao wamekuwa hawafurahii mambo makubwa yakimaendeleo na ya kujivunia yanayofanywa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli, kwani kwa namna moja ama nyingine yamekuwa yakigusa maslahi yao.
VIDEO: