Vita ya Namba Taifa Stars, Kenya Leo ijipange..Lazima Wachezee Kichapo
0
July 28, 2019
Dar es Salaam. Ushindani wa nafasi kwa baadhi ya wachezaji wa timu ya taifa ‘Taifa Stars’ unaweza kuwa chachu ya mafanikio kwenye mechi yao ya kuwania kufuzu fainali za CHAN dhidi ya Kenya ‘Harambee Stars’ leo jioni kabla ya kurudiana tena Agosti 4.
Kufikia sasa zipo baadhi ya nafasi ambazo zinaonekana zitaliumiza kichwa benchi la ufundi katika upangaji wa kikosi kutokana na ubora na viwango ambavyo wachezaji wa nafasi husika wamekuwa wakionyesha kwenye mazoezi ya kipindi hiki cha maandalizi.
Ushindani wa kwanza ambao huenda ukainufaisha Stars ni ule uliopo kwenye nafasi ya kipa kati ya Aishi Manula na Juma Kaseja.
Manula ndiye amekuwa kipa chaguo la kwanza kwa muda mrefu, lakini uwepo wa Kaseja ambaye amekuwa akionyesha kiwango kizuri kwenye ligi na hata mazoezini Stars, unaleta matumaini kwamba lango la timu liko salama kwenye mechi ya kesho.
Kaseja ni mzoefu na amekuwa na uwezo wa hali ya juu katika kuipanga timu kama ilivyo kwa Manula, lakini yeye ana faida ya ziada ya kuwa na uwezo wa kucheza mipira ya krosi ambayo imekuwa ikimsumbua Aishi.
Nafasi nyingine ambayo inaonekana itaisaidia Stars kwenye mchezo huo kutokana na ushindani wa wachezaji wake ni ile ya beki wa kushoto inayochezwa na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ na Gadiel Michael ambao wote wawili wamekuwa wakitajwa kama mabeki bora wa kizazi cha sasa nchini.
Mbali na hao, ushindani baina ya Frank Domayo na Salum Abubakar unaweza kuleta ufanisi katika eneo la kiungo cha ushambuliaji ambacho ndiyo jiko la mabao Stars.
Kwenye eneo la ushambuliaji nahodha John Bocco anayecheza nafasi ya mshambuliaji wa kati, atapaswa kujipanga na kuhakikisha anakuwa na ufanisi wa hali ya juu kwani anaweza kujikuta anapoteza nafasi mbele ya Salim Aiyee aliyeshika nafasi ya pili kwa kufumania nyavu kwenye Ligi Kuu msimu uliopita au Iddi Seleman ‘Nado’ aliyepachika mabao 10 msimu uliopita akiwa na Mbeya City kabla ya kujiunga na Azam msimu huu.
Kocha wa Stars, Etienne Ndayiragije alisema anaamini kila mchezaji aliyepo kikosini ana nafasi ya kutoa mchango kwenye timu hiyo.
PIGO HARAMBEE STARS
Kenya ambayo ilianza kujifua mapema kwa mechi ya kesho tangu ilipotolewa kwenye AFCON kule nchini Misri, imepata pigo baada ya nyota wake wawili winga tegemeo Paul Were na straika wa Sofapaka, John Avire kuthibitika wakaikosa mechi hiyo kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo ya kukimbizia dili za uhamisho.
Kocha Sebastien Migne amethibitisha kuwakosa nyota hao.
Mwananchi
Tags