Zaidi ya wahamiaji 100 waliokuwa wakielekea Ulaya hawajulikani waliko na inahofiwa wamekufa maji baada ya boti walizokuwa wakisafiria kuzama katika pwani ya Libya.
Hayo yamesemwa na Shirika la Wahamiaji la Umoja wa Mataifa, IOM, pamoja na walinzi wa pwani nchini Libya.
Ayoub Gassim, ambaye ni msemaji wa walinzi wa pwani nchini Libya, ameliambia shirika la habari la Associated Press kuwa boti mbili zilizowabeba takriban wahamiaji 300 zilizama yapata kilomita 120 mashariki mwa mji mkuu wa Libya, Tripoli.
Ameongeza kuwa wahamiaji 137 waliokolewa na kurudishwa Libya, lakini hadi sasa walinzi wa pwani wamefaulu kuopoa mwili mmoja pekee.
Charlie Yaxley ambaye ni msemaji wa Shirika la Wakimbizi la Umoja wa Mataifa, UNHCR, amesema wanakadiria kuwa wahamiaji 150 miongoni mwao wanawake na watoto, hawajulikani waliko na wanahofiwa kufa maji.