Wananchi Ambao Sauti zao zimedukuliwa Wametakiwa Kwenda Mahakamani


Mratibu wa Mtandao wa watetezi wa haki za binadamu (Thrdc), Onesmo Olengurumwa akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo, wakati akitoa tamko la mtandao huo kuhusu mazungumzo ya faragha na usalama wa mawasiliano nchini. Kulia ni Wakili na Afisa Utetezi wa mtandao huo, Leopold Mosha. Picha na Ericky Boniphace

Dar es Salaam. Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC) umewataka watu ambao sauti zao zimedukuliwa na kusambazwa mitandaoni kufungua kesi mahakamani.

Umesema kesi hizo zikifunguliwa, wahusika wanaweza kuwashtaki watu au taasisi wanazodhani kuhusika kwa maelezo kuwa kitendo hicho ni kinyume na katiba ya Tanzania.

Wito huo umetolewa leo Jumapili Julai 28, 2019 19  na mratibu wa mtandao huo,   Onesmo Olengurumwa  katika mkutano wake na waandishi wa habari.

Katika mkutano huo, Olengurumwa amesema usalama na faragha ya mawasiliano ni moja ya haki inayokiukwa kwa kasi nchini na kwingineko duniani.

Ametoa kauli hiyo kipindi ambacho katika mitandao ya kijamii zimesambaa sauti zinazodaiwa kuwa za makada wa CCM, wanaosikia wakizungumzia masuala mbalimbali na kuzua hali ya sintofahamu.

Wanachama wa vyama hivyo waliibuka na kutaka ufanyike uchunguzi kwa wanaodaiwa sauti zao kusikika, wapo waliolaani kitendo hicho na  baadhi ya wahusika wakisema jambo hilo viachiwe vyombo vya usalama kuchunguza.

Olengurumwa amesema hivi  karibuni zimesambaa taarifa ya kudukuliwa kwa mawasiliano ya watu na kusambazwa mitandaoni.

“Wahanga wakubwa ni viongozi wa Serikali wastaafu na vyama vya siasa, watu wengi wanaamini ni kweli kwa kuwa hakuna aliyejitokeza kukemea endapo zilikuwa ni sauti za kutengenezwa.”

"Suala la mawasiliano binafsi limelindwa kikatiba na kisheria kama haki ya faragha, zipo mamlaka ambazo zimeruhusiwa na sheria kuweza kuchukua taarifa binafsi za mtu kwa matumizi maalamu  lakini hazipaswi kubadilika kuwa za umma," amesema Olengurumwa.

Amesema taarifa za mtu zinapaswa kutolewa kwa kibali cha mahakama kwa matumizi maalumu, hivyo jamii inapaswa kujiepusha na usambazaji wa taarifa hizo kwa kuwa ni kinyume na sheria.

Mwananchi
Tags

Post a Comment

1 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.
  1. Hiyo ndiyo sahihi: kwenda mahakamani.
    Wanaodai eti sheria ibadilishwe kulinda faragha za watu nia yao ni mbaya wanataka walindwe katika mabaya yao usaliti, uhaini na kadhalika mambo ambayo si mazuri kwa maslahi ya taifa. Ni vyema hayo mabaya yakaendelea kudukuliwa kulinusuru taifa.
    UsirudieKosaKupigiaKuraUpinzaniOvyo!

    ReplyDelete

Top Post Ad

Below Post Ad