Suala ufanyaji wa mikutano ya kisiasa limeibua mjadala mpya kwa wananchi mbalimbali kufuatia baadhi ya wanasiasa kufanya mikutano yoyote ya kisiasa bila zuio ilhali wengine wakikumbana na zuio kutoka Jeshi la Polisi.
Hali hiyo imekuja baada ya Katibu Mkuu wa CCM, Dkt. Bashiru Ally kuonekana akifanya mikutano ya ndani bila zuio lolote wakati huo huo wanasiasa wa upinzani wakizuiwa, huku wananchi wakitolea mfano wa Mbunge wa Kawe Halima Mdee ambaye hivi karibuni alizuiwa kufanya mkutano wa ndani mkoani Kagera.
Kwa mujibu wa gazeti la Mwananchi baadhi ya wananchi waliozungumza gazeti hilo wamesema jambo hilo linaweza kuwagawa kwa kuwa halionyeshi usawa katika ulingo wa siasa, wengine kusema ni sawa kwa viongozi wa CCM kutozuiwa kwa kuwa chama hicho ndio kinaongoza Serikali.
Wakati wananchi wakieleza hayo Julai 9, 2019 Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi alisema ofisi yake haijawahi kupokea malalamiko ya maandishi kutoka vyama vya upinzani kuhusu kuzuiwa kufanya mikutano ya hadhara.
Kauli ya Jaji Mutungi ilithibitishwa na katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji ambaye amesema chama chake hakijawahi kufanya hivyo, akiamini hilo lipo juu ya uwezo wake.
Jaji Mutungi alitoa kauli hiyo baada ya kuulizwa na Mwananchi kuhusu malalamiko yanayotolewa na vyama vya upinzani kuzuiwa kufanya mikutano hiyo huku CCM ikiruhusiwa.
Julai 6, 2019 Dk Bashiru Ally alianza ziara ya siku nne mkoani Kilimanjaro na baadaye kuelekea Manyara, mikutano inayofanana na ya baadhi ya viongozi wa vyama vya upinzani lakini wamekuwa wakizuiwa.
Julai 13, 2019 Mdee ambaye pia ni mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la Chadema (Bawacha) akizuiwa kufanya mkutano wa ndani wilayani Bariadi Mkoa wa Simiyu ambao ulitawanywa kwa mabomu ya machozi na polisi.
Julai 14, 2019 Mdee alipokuwa mkoani Kagera alikamatwa na polisi na kuwekwa ndani siku mbili.
Mkazi wa Tabata Segerea mtaa wa Mzimuni, Abdulfatah Lyeme amesema vyama vyote vya siasa vinatakiwa kufanya siasa kwa uhuru na haki kama inavyoonekana kwa CCM.
Dereva bodaboda eneo la Ubungo Jijini Dar es Salaam, Rishandumi Ndosi amesema jambo la kuzuia mikutano ya upinzani ni ukandamizaji, “Wasitake kuonekana wao tu hata wapinzani wanataka wauze sera zao, sasa kuwakandamiza siyo sawa kwa sababu ile amshaamsha ya upinzani imesaidia hata wao kubadilika.”
Mama Lishe mkazi wa Arusha Mjini, Zainabu Suleiman amesema hakuna sababu ya kuendelea kushindana na mshika mpini na kwamba kinachohitajika ni utulivu kulinda usalama.
Mkazi mwingine wa Tabata, Gasto Mlay amesema kwa sasa kitendo cha kuzuia upinzani kinajenga chuki kwa Watanzania.
“Yaani mimi nashangaa kwa sababu katiba ni moja , sheria ipo lakini wapinzani wanazuiliwa halafu CCM ndiyo wanafanya siasa wao tu, hiyo inasikitisha sana, Serikali inatakiwa iondoe hali hii,” amesema Mlay.
Joseph Bigaro amesema hakuna sababu ya kulalamikia kuwa CCM wanapendelewa wakati chama hicho tawala ndio kinatekeleza ahadi zake kwa wananchi.
“Anayeongoza nchi ni nani si ni CCM? Sasa wakizunguka kufanya mikutano ni haki yao maana wanadaiwa na wananchi, hao wapinzani wanadaiwa nini, waliahidi nini. Nadhani kwa maoni yangu sioni tatizo kabisa la upendeleo,” amesema, Bigaro ambaye ni mkazi wa Morogoro.