Watanzania na Wakenya ni miongoni mwa 26 waliouawa katika shambulizi Somalia


Idadi ya watu waliouawa katika shambulio la kigaidi dhidi ya hoteli moja kusini mwa Somalia imeongezeka na kufikia watu 26. Awali Polisi ya Kismayo iliripoti kuwa waliouawa katika hujuma hiyo ya kigaidi ni watu saba.

Rais wa eneo lenye mamlaka ya ndani la Jubaland kusini mwa Somalia, Ahmed Mohamed amesema miongoni mwa waliouawa katika shambulio hilo la kigaidi la jana Ijumaa katika mji wa bandari wa Kismayo ni raia kadhaa wa Tanzania, Kenya, Marekani na Uingereza.

Vyombo vya usalama vinasema kuwa, gaidi mmoja aligongesha gari lililojaa mada za milipuko katika Hoteli ya Asasey katika mji wa Kismayo kabla ya washambuliaji hao kuvamia jengo hilo.

Msemaji wa operesheni za kijeshi wa kundi la wanamgambo wa al-Shabaab, Abdiasis Abu Mus'ab ametangaza kuwa, wanachama wa genge hilo ndio waliohusika na shambulizi hilo.

Shambulio hilo limefanyika siku moja baada ya kumalizika mkutano wa kupiga vita ugaidi uliofanyika katika mji mkuu wa Kenya, Nairobi, ambapo mikakati ya kulitokomeza kundi hilo la ukufurishaji ilijadiliwa.

Akihutubu katika mkutano huo wa Pan African counter-terrorism, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa, Antonio Guterres alionya kuwa ugaidi unatishia amani ya bara la Afrika na kusisitiza kuwa, jinamizi hilo halipaswi kuruhusiwa kudhoofisha mwenendo wa ustawi katika bara hilo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad