Waziri Lugola aagiza Polisi kuwakamata wanaowapa mimba Wanafunzi

Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola, amelitaka Jeshi la Polisi  wilayani Bunda, mkoani Mara, kuwakamata wazazi wanaowatumia wanafunzi katika shughuli za kilimo na mifugo na kuwasababishia kukatisha masomo yao.

Pia Waziri Lugola amewaagiza Polisi hao kuwakamata watu wanaowarubuni wanafunzi wa kike na kuwasababishia kukatisha masomo kwa kuwapa mimba.

Waziri Lugola, ametoa kauli hiyo akiwa wilayani Bunda katika  ziara ya kutembelea miradi ya maendeleo ndani ya jimbo lake la Mwibara, ambapo amesema kuwa lazima Watoto waendelezwe kielimu ili iwaletee manufaa kwao na kwa taifa.

“Nina taarifa baadhi ya wazazi uwatumikisha Watoto wao kufanya shughuli za kilimo, kulima dengu, pamoja na kuwatumia katika kuchunga mifugo, hii haikubaliki, wazazi lazima muwajibike kwa kutowatendea vema watoto,” alisema Lugola na kufafanua;

“Kuvunja sheria za nchi kwa kutompa elimu mtoto ni kosa, hivyo, wazazi wanaotumikisha Watoto shughuli za uchumi wa wazazi hao,hakika tutawakamata, OCD (Kamanda wa Polisi Wilaya), akikisheni mnawakamata wazazi ambao wanawatumia Watoto katika shughuli zao binafsi na pia kusababisha utoro katika shule zetu.”

Pia Lugola aliwahoji wanafunzi wa Shule ya Msingi Karukekere, Kata ya Namuhura, Wilayani humo, kuwa wanataka Serikali iwafanyie nini wazazi wao ambao wanawakatisha masomo, hata hivyo,wanafunzi hao walisema wazazi wao washitakiwa kwa kutowapa haki zao za msingi.

Alisema ili kupunguza utoro ndani ya Jimbo hilo, aliwataka wazazi kufuatilia elimu ya watoto wao, kwa kuhakikishe wanakua na daftari ambalo wanafunzi hao wataenda nalo shuleni, na Mwalimu atasaini baada ya mwanafunzi huo kufika shuleni na pia atasaini kabla ya muda wa kuruhusiwa kwenda nyumbani, hatua hiyo itapunguza zaidi utoro katika jimbo lake.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad