WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema atamtuma Waziri wa Nchi katika Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Sera, Uratibu, Kazi, Ajira na wenye Ulemavu, Bi. Jenista Mhagama aende Makanya, wilayani Same, kwenye mashamba ya mkonge akatatue kero za wafanyakazi.
“Nitamleta Waziri wa Nchi anayesimamia masuala ya kazi, aje afuatilie kero za wafanyakazi hapa Makanya, manake watumishi wameweka malalamiko yao kwenye mabango na mimi nimeona wanaoendesha mitambo hawana gloves, wengine wamevaa kandambili badala ya mabuti, kofia za usalama nimeambiwa ziko 20 tu…” alisema Waziri Mkuu.
Ametoa ahadi hiyo jana (Ijumaa, Julai 19, 2019) wakati akizungumza na wafanyakazi wa kiwanda cha kuchakata katani kilichopo kwenye shamba la mkonge la Hasani, kata ya Makanya, wilayani Same, Kilimanjaro, mara baada ya kukagua uzalishaji kwenye kiwanda hicho.
Alifikia uamuzi huo baada ya kusoma mabango yaliyokuwa yakitoa ujumbe juu ya hali mbaya kiwandani zikiwemo malipo ya sh. 3,800 kwa siku; mikataba mibovu ya kazi; wafanyakazi kutothaminiwa wanapougua na kutoridhika na mawakala wawili ambao ni UNIQUE na UPANI waliowekwa kusimamia uendeshaji wa shamba hilo. UNIQUE inasimamia wakata mkonge na UPANI inasimamia kazi ya upandaji na upanuzi wa mashamba.
Hata hivyo, Waziri Mkuu alimweleza Meneja wa Mashamba ya METL likiwemo la Hasani, Bw. Ndekiwa Nyari kwamba uamuzi wa kuweka mawakala unawapunguzia wenye kampuni mzigo wa usimamizi kwenye mashamba lakini unaipa hasara kampuni yao.
“Kwa sasa unashughulika na watu watatu au wanne ambao ni mawakala wakati watu wote wanaokuzalishia wako hapa. Ni vema ungeajiri hao watu wanne, ukawasimamia kwa karibu na unaweza kuwapa motisha wakifanya vizuri au kuwafukuza wakiharibu. Lakini kwa sasa hawa mawakala huna mamlaka hayo, sababu ulishaweka mkataba nao,” alisema.
“Ni bora uwe na idara mbili za upandaji na uvunaji, kisha uweke wasimamizi watatu au wanne ambao watawajibika kwako moja kwa moja. Hii system uliyotumia ina walakini hasa kwenye maslahi ya wafanyakazi. Unawalipa fedha lakini haifiki yote kwa wafanyakazi,” alisema na kuamsha shangwe miongoni mwa wafanyakazi hao.
Wakati huohuo, Waziri Mkuu alitumia fursa hiyo kuwataka wananchi wa Makanya wajipange na kutafuta maeneo ya ekari tatu hadi nne ili nao waanze kulima mkonge ambao alisema watakuwa wanauuza kwenye kiwanda hicho.
“Niwasihi wananchi wa hapa na vijiji jirani ingieni kwenye kilimo cha mkonge kwa sababu kina soko ndani na nje ya nchi. Tafuteni maeneo ya ekari tatu au nne anzisheni kilimo cha mkonge sasa. Zao hili lipo kwenye mazao ya nyongeza ya mkakati ambayo ni chikichi na mkonge.”
“Na uzuri wake unalima mara moja tu, halafu kila mwaka unakuwa unavuna tu. Viongozi wa Serikali ya Kijiji simamieni jambo hili,” alisisitiza.
Mazao mengine ya mkakati ambayo Serikali ya awamu ya tano ilianza kuyatilia mkazo ili kuimarisha uzalishaji wake, upatikanaji wa pembejeo na masoko ni pamba, chai, tumbaku, kahawa na korosho.
Mapema, akitoa taarifa juu ya uzalishaji kwenye kiwanda hicho, Bw. Nyari alisema shamba lote lina ukubwa wa ekari 2,453 na kwamba uzalishaji umekuwa ukiongezeka kidogo kidogo ambapo mwaka 2014 walizalisha tani za mkonge 713 na hadi kufikia mwka 2018 walifikisha tani 890 za mkonge. “Mwaka huu tunatarajia kufikisha tani 1,080 kwa sababu eneo lililopandwa mkonge limeongezeka,” alisema.
Alisema moja ya changamoto inayowasumbua ni tabia ya wafugaji kuingiza mifugo kwenye mashamba yenye mkonge mchanga hali ambayo alisema inaua miche hiyo michanga.
Aliitaja changamoto nyigine kuwa ni ukosefu wa maji ya uhakika, hali ambayo inawafanya washindwe kuzalisha singa za katani ambazo ni safi.
Waziri Mkuu leo anaendelea na ziara yake mkoani Kilimanjaro kwa kutembelea wilaya ya Mwanga ambako atazungumza na watumishi na kisha ataenda kijiji cha Kirya, Nyumba ya Mungu kukagua mradi wa maji wa Same - Mwanga - Korogwe.
(mwisho)
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,