Waziri Mpango aieleza UN utekelezaji malengo 17

Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Philip Mpango amewasilisha ripoti ya Tanzania kwa mara ya kwanza ya Mapitio ya Hiyari ya Utekelezaji wa Malengo ya Maendeleo Endelevu katika Mikutano ya Jukwaa la Juu la Kisiasa la Ngazi za Mawaziri chini ya Umoja wa Mataifa inayofanyika New York, Marekani.

Akiwasilisha ripoti hiyo Waziri Mpango ameeleza kuwa Tanzania imefanikiwa katika utekelezaji wa malengo 17 yaliyoamuliwa kutekelezwa na nchi zote ulimwenguni ili kuondokana na umasikini na kuharakisha maendeleo katika nyanja zote.

Akizungumzia lengo namba nne lenye kuangazia elimu jumuishi na bora kwa wote, Dk Mpango alieleza kuwa Tanzania imepiga hatua katika uandikishaji wa wanafunzi wa darasa la kwanza ambao wana mwaka mmoja wa elimu ya awali kwa asilimia 95.6 mwaka 2018 ambayo ni juu ya makadirio ya asilimia 87.5 ifikapo mwaka 2020. Aidha, wanafunzi wanaojiunga na kidato cha kwanza wameongezeka kwa asilimia 17.4, ikiwa ni kutokana na mafanikio ya elimu bure chini ya Serikali ya Awamu ya Tano.

Pia aliongeza kuwa Tanzania imefanikiwa katika maeneo ya utoaji huduma bora za afya, uongozi bora na amani ya nchi kwa ujumla. Ripoti hiyo imepokewa vizuri katika Jukwaa hilo la Umoja wa Mataifa ambapo nchi zilizotoa maoni kuhusu ripoti hiyo ikiwemo Kenya zimepongeza juhudi zilizofikiwa na Tanzania katika utekelezaji wa malengo endelevu.

"Malengo haya ndio dira ya maendeleo na yanaunganika na mipango yetu ya maendeleo kwa pande zote za Jamhuri ya Muungano wa Tanzania yanaendana na Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa Miaka Mitano, na MKUZA kwa upande wa Zanzibar hivyo ni lazima tutekeleze malengo haya kwa bidii, alisema Waziri Mpango.

Dk. Mpango alitoa mwito kwa Jumuiya ya Umoja wa Mataifa na nchi zenye utaalamu kuisaidia Tanzania katika matumizi ya teknolojia ili kuweza kufikia azma ya malengo endelevu upande wa utunzaji wa mazingira.

Aliwashukuru wadau wote, sekta binafsi na taasisi zisizo za kiserikali kwa ushiriki wao katika kuandaa ripoti hiyo kwa kiwango kizuri. Aidha alitoa mwito kwa taasisi na sekta binafsi kushirikiana na serikali katika kuhakikisha kuwa rasilimali fedha na utaalamu zitumike kwa ajili ya kushughulikia utekelezaji wa malengo endelevu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad