KAMPUNI ya WhatsApp inayoendesha huduma ya mawasiliano ya kutumiana ujumbe ina mpango wa kuzindua huduma yake ya kwanza ya malipo nchini India, nchi ambayo ni soko lake kubwa likiwa na watumiaji wapatao milioni 400, ilisema taarifa ya kampuni hiyo.
WhatsApp inayomilikiwa na kampuni ya Facebook imeanza majaribio ya huduma hiyo kwa watu zaidi ya milioni moja mwaka jana. Lakini uzinduzi rasmi bado haujafanyika ukisubiri kuidhinishwa na taasisi inayoratibu huduma za benki.
“Malipo ya WhatsApp yatarahisisha kumlipa mtu kwa njia ya WhatsApp kama anavyotuma fedha, tunasubiri kwa hamu kuanza kutoa huduma hii kwa watumiaji wetu kote nchini India,” kiongozi wa kampuni hiyo , Will Cathcart, alisema katika taarifa yake.
Nchi ya India itakuwa nchi ya kwanza kuanza kutumia malipo ya WhatsApp, huduma hiyo itakapozinduliwa. WhatsApp itaingia katika soko la ushindani na kampuni nyingine za malipo ya kidijitali za Amazon Pay na Google Pay.