UONGOZI wa Yanga umekamilisha taratibu za usajili wa beki wa kushoto wa Rayon Sports ya Rwanda, Ericky Rutanga anayejiunga na timu hiyo kwenye usajili wa dirisha dogo Ligi Kuu Bara maalum kwa ajili ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Awali, Yanga iliwahi kumfuata beki huyo na kuzungumza naye na kushindwa kufikia muafaka mzuri na kusalia Rayon huku Gadiel Michael aliyekuwa akicheza nafasi hiyo, naye akitimkia Simba.
Yanga mara baada ya kushindwana na beki huyo haraka ikakamilisha usajili wa beki wa Singida United, Muharami Salum maarufu kwa jina la Marcelo ambaye tayari yupo kambini mkoani Morogoro.
Yanga msimu ujao itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika iliyo chini ya Shirikisho la Soka Afrika ‘Caf’ ambapo itaanzia hatua ya awali iliyopangwa kuanza Agosti 9, mwaka huu na michuano hiyo itamalizika Mei 30, mwakani.
Hivyo basi kama itafanikiwa kushinda mechi za awali za mtoano na kutinga hatua ya makundi, basi itapewa nafasi ya kuongeza wachezaji. Kwa mujibu wa taarifa ambazo imezipata Championi Jumamosi, Rutanga rasmi atajiunga na Yanga kwenye usajili wa dirisha dogo akiwa kama mchezaji huru baada ya mkataba wake kumalizika.
Habari zinasema kwamba beki huyo atajiunga na Yanga katika usajili huo kuchukua nafasi ya mchezaji wa kigeni, Klaus Kindoki aliyekataa kutolewa kwa mkopo huku akisubiria mkataba wake kumalizika kipindi hicho.
“Rutanga tayari amemalizana na Yanga kwa asilimia 70 na anajiunga nayo kwenye usajili wa ligi na atakuja kuchukua nafasi ya Kindoki ya wachezaji wa kigeni.
“Kama unavyofahamu nafasi za wachezaji wa kigeni tayari zimefikia kumi kama idadi ambao TFF wanaitaka, hivyo wakati Kindoki anaondoka baada ya mkataba wake wa miezi sita kumalizika na Rutanga atakuwa amekuja Yanga.
“Kikubwa uongozi unataka kuwa na mchezaji mwenye uzoefu na uwezo wa michuano ya kimataifa ambayo Yanga watashiriki, mwaka huu,” alisema mtoa taarifa huyo.