Zungu la Dawa za Kulevya Duniani ‘El Chapo’ Ahamishiwa Gereza Lingine Hatari Zaidi Marekani, Hofu yatawala

Gwiji la mtandao wa biashara za madawa ya kulevya duniani,  Joaquin Guzman almaarufu kwa jina la El Chapo amehamishiwa gereza lingine lenye ulinzi mkali zaidi nchini Marekani la ADX Florence la mjini Colorado.


Guzman alihukumiwa kifungo cha maisha jela na miaka mingine 30 siku ya Jumatano ya wiki hii baada kukutwa na makosa ya biashara ya dawa za kulevya na kushiriki njama za mauaji wakati akiwa kiongozi wa genge kubwa zaidi la biashara hiyo la Sinaloa.

Taasisi inayosimamia magereza nchini Marekani (MCC) imethibitisha taarifa hiyo, Na kueleza kuwa ni kutokana na rekodi mbaya ya kutoroka magerezani kwa mfungwa huyo.

El Chapo (62) aliwahi kutoroka mara mbili kwenye magereza yenye ulinzi mkali nchini Mexico mwaka 2001 na 2015, Kabla ya kukamatwa tena mwaka 2017.

Gereza la ADX Florence lina wafungwa 375 na lilifunguliwa mwaka 1994. Imeelezwa kluwa ndio gereza linalofungwa watukukutu wote wanaoisumbua Marekani na dunia kwa ujumla, Na hakuna mfungwa aliyewahi kutoroka.

Hukumu ya kesi hiyo iliyosikilizwa na mahakama ya serikali kuu ya Brooklyn, New York iliangazia kisa cha mtu mmoja aliyearifu kwamba alinusurika kuuawa katika shambulizi lililopangwa na Guzman.

Mwezi Februari mwaka huu, Guzman, 62 alikutwa na hatia ya kufanya biashara haramu ya maelfu ya tani ya dawa za kulevya aina ya cocaine, heroin na bangi, pamoja na kujihusisha na kupanga matukio kadhaa ya mauaji, wakati akiwa kama kiongozi wa genge la Sinaloa.

Genge hilo  kwa muda mrefu lilitambulika kuwa genge kubwa zaidi miongoni mwa mengine, lenye ubabe na linalouza madawa kwa wingi zaidi duniani.

Kabla ya hukumu hiyo waendesha mashitaka walimwomba jaji wa mahakama ya wilaya, Brian Cogan kumuhukumu kifungo cha maisha gerezani, pamoja na miaka 30 ya kutumia silaha za moto.

Awali kabla ya hukumu hiyo, Guzman ambaye jina lake linamaanisha “Mfupi” alikuwa kizuizini, katika chumba alichofungiwa peke yake kwenye gereza la Metropolitan, lenye muundo wa ngome huko Manhattan.

Mwezi uliopita, jaji Cogan alitupilia mbali ombi la Guzman la kufanya mazoezi kwenye dari ya gereza hilo, baada ya waendesha mashitaka kusema anaweza kutumia upenyo huo kutoroka.

Alifanikiwa zaidi kibiashara miaka ya 1990 hadi 2000, kupitia vita vya mara kwa mara na wapinzani wake, na hatimaye kuja kujulikana zaidi kama kiongozi wa genge hilo la Sinaola.

Guzman anatajwa kuwa ndiye mtu muuza madawa mwenye ushawishi zaidi kuwahi kutokea baada ya Mkolombia Pablo Escobar aliyeuawa mwaka 1993.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad