Rais wa zamani wa Zimbabwe, Robert Mugabe mwenye umri wa miaka 95 imekuwa gumzo baada ya picha zinazomuonesha akiwa amekaa kwenye kiti cha wagonjwa chenye matairi kusambaa.
Picha hizo zilisababisha gumzo kwenye mitandao ya kijamii, hasa kutokana na kutomuona hadharani kwa kipindi kirefu mpigania uhuru na muasisi wa taifa hilo.
Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa amezungumzia afya ya mtangulizi wake, akieleza kuwa alikuwa amelazwa hospitalini nchini Singapore tangu Aprili mwaka huu.
Alisema kuwa Mzee Mugabe, Rais wa kwanza wa taifa hilo anaendelea vizuri na kwamba anaweza kuruhusiwa kutoka hospitalini muda wowote.
Hii ni mara ya pili Rais Mnangagwa anazungumzia afya ya Mugabe kwa umma bila kutaja ugonjwa unaomsibu.
Novemba mwaka jana, Rais Mnangagwa alisema kuwa mtangulizi wake huyo hawezi kutembea kutokana na maradhi na uzee. Alisema kwa sasa analazimika kuwa chini ya uangalizi wa daktari kwa muda mrefu zaidi ya ilivyokuwa awali.
Mugabe aliiongoza Zimbabwe kwa kipindi cha miaka 38, hadi mwaka 2017 alipolazimika kujiuzulu baada ya watu kuandamana na jeshi kuingilia kati.