Mwanaharakati msomi nchini Uganda, Dkt. Stella Nyanzi amehukumiwa kwenda jela mwaka mmoja na nusu kwa kosa la kumtolea lugha chafu Rais wa nchi hiyo, Yoweri Kaguta Museveni.
Nyanzi amekutwa na hatia ya unyanyasaji wa kimtandao pamoja na mawasiliano ya udhalilishaji dhidi ya rais Yoweri Museveni na familia yake.
Aidha, kabla ya hukumu hiyo, Dkt. Nyanzi alikataa kumsikiliza hakimu wakati akisoma hukumu dhidi yake na badala yake kufanya vurugu kwa kuvua nguo na kuonesha sehemu ya mwili wake.
Wakati kesi ikiendelea, Dkt. Nyanzi alikataa kuomba dhamana na amekuwa katika gereza kuu la Uganda la Luzira kwa miezi minane tangu akamatwe.
Pia Dkt. amekuwa mtu maarufu sana nchini humo ambaye amekuwa akitumia lugha chafu kuukosoa hadharani utawala wa Rais Museveni kwa kuandika katika mitandao ya kijamii maneno yasiyokuwa na staha kuhusu utawala wa Rais huyo.
Dkt. Nyanzi ambaye ni mtafiti wa masuala ya jamii, kabla ya kuanza kampeni yake ya matusi kupitia kwenye mitandao ya kijamii aliwahi kuwa mhadhiri katika chuo kikuu cha umma nchini Uganda cha Makerere.
Hata hivyo, mashtaka hayo chini ya sheria ya matumizi mabaya ya kompyuta ni jaribio la utekelezwaji wa sheria ya uhalifu wa mtandaoni inayokosolewa na wengi.