Waziri wa Habari, Sanaa, Utamaduni na Michezo, Dk Harrison Mwakyembe, amelitaka Shirikisho la soka nchini (TFF), kuzingatia masharti yaliyopo kwenye mkataba wa udhamini wa ligi kuu.
Mwakyembe ameyasema hayo jana usiku kwenye hafla ya kusaini mkataba wa miaka 3, wenye thamani ya shilingi Bil 9, iliyoingia TFF na kampuni ya simu za mkononi Vodacom.
''Makubaliano mliyosaini hapa yana masharti yake, naomba TFF mzingatie ili kuendelea kuwa kivutio kikubwa kwa makampuni mengine kuwa wadhamini wadogo wa ligi baada ya kupata mdhamini mkuu'', amesema.
Aidha Mwakyembe ameongeza kuwa soka la Tanzania litaendelea kukua, kwa viongozi kuwa makini kama ilivyo kwa uongozi wa sasa wa TFF, kwani hakuna mwekezaji ambaye yupo tayari kusaini mkataba na watu wa hovyo hovyo.
Vodacom watadhamini ligi kuu kwa miaka mitatu mfululizo kama mdhamini mkuu, kwa kutoa shilingi Bil 3 kila msimu. Ikumbukwe ligi kuu msimu uliopita ilichezwa bila kuwa na mdhamini mkuu.