Bashe ataka Bodi ya nafaka na mazao mchanganyiko kuwa kiungo cha biashara ya mazao Baina ya Kenya na Tanzania



NAIBU Waziri wa Kilimo, Mhe. Hussein Bashe amesema kikao cha kwanza baina ya timu ya wataalamu wa masuala ya Mazao ya Chakula hapa nchini ikiongozwa na Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB) na ya wenzao kutoka Kenya zinakutana hapa nchini leo Agosti 17, 2019 ili kujadiliana namna bora ya kufanya biashara ya mazao hayo.

Akizungumza na waandishi wa habari jana usiku Agosti 16, 2019 kwenye ofisi za Kituo cha Uwekezaji Nchini (TIC), jijini Dar es Salaam, Mhe. Bashe alisema, kikao hicho ni makubaliano baina ya nchi hizo mbili kukutana na kujadili namna gani wafanyabiashara wa Kitanzania na wenzao wa Kenya watafanya  biashara ya mazao ya chakula na iwe biashara endelevu.

“Biashara tayari imekwisha anza na wakati tunaendelea mpaka sasa wenzetu wa Kenya wamekwishanunua jumla ya tani 34,000 kupitia kwa wafanyabiashara wetu na biashara hiyo inaendelea.” Alifafanua.

Alisema timu ya wataalamu kutoka Tanzania itaongozwa na watu kutoka Wizara ya Kilimo, Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko (CPB), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) na Mamlaka ya Viwango Tanzania (TBS) ili wakae chini na wakubaliane utaratibu wa namna gani  wafanyabiashara wa Tanzania na wenzao wa Kenya watafanya biashara ya mazao ya chakula.

“Sisi Wizara ya Kilimo jukumu letu ni kufanya mambo makubwa mawili, kuhamasisha uzalishaji wa mazao na kufungua masoko ya wakulima wetu ili waweze kufanya biashara.” Alifafanua.

Alisema katika kikao hicho wametaka mamlaka za viwango za Kenya na Tanzania zijumuishwe kwenye majadiliano hayo ili wazalishaji wa sembe waliosajiliwa Tanzania waweze kusajiliwa Kenya Bureau of Standards ili bidhaa zao ziweze kwenda katika soko la Kenya bila vikwazo vyovyote.

“Tunatengeneza Government Agreement ambayo itaonyesha mpango kazi (frame work) ya namna biashara hii itafanyika, tumeshaiteua Bodi ya Nafaka na Mazao Mchanganyiko ambayo ndiyo itakayokuwa kiongozi msimamizi na kiungo wezeshi katika biashara hiyo.” Alibainisha Mhe. Bashe.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad