Chadema yataka Rais Magufuli Kumchukulia Hatua RC Charamila
0
August 31, 2019
Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kinapinga, kukemea na kulaani vikali kwa nguvu zote, kauli zinazokiuka na kutishia haki za binadamu, ikiwemo kuhamaisha na kuagiza mauaji ya watu wasiokuwa na hatia, za Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Albert Charamila.
“Tunatoa wito kwa mamlaka ya uteuzi wake kuchukua hatua za haraka za kumwadhibu vinginevyo itachukuliwa kwa uzito mkubwa kuwa kauli hizo ni msimamo unaoungwa mkono na kubarikiwa na Serikali ya CCM chini ya Rais John Magufuli,”
Kwa siku mbili mfululizo, jana na leo, mkuu huyo wa mkoa ambaye kwa nafasi yake ni mwakilishi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika eneo hilo la utawala na Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, amenukuliwa katika njia mbalimbali akitoa kauli hatarishi kwa haki za binadamu, zikihamasisha mauaji ya watu, kinyume cha taratibu za nchi, kama zinavyoelekezwa na Katiba ya Nchi.
Kupitia mitandao ya kijamii ya vyombo vya habari nchini na kwenye video fupi zinayosambaa kwenye mtandao wa WhatsApp, Ndugu Charamila amenukuliwa akitoa kauli;
1. Za kuhamasisha watu wasiokuwa na hatia wapigwe na kuuwawa.
2. Za kuagiza na kuamrisha vyombo vya ulinzi na usalama kupiga na kuua watu wasiokuwa na hatia.
3. Zinanoonekana kuwa za kujivunia na kujipongeza kwa kupiga au kutesa au kuua mtu, kinyume na taratibu za nchi yetu.
Katika hatua hii, mbali ya kukemea, kulaani na kupinga vikali kauli hizo za Charamila, ambazo ni mwendelezo wa kauli zake nyingine zinazoashiria kuwepo kwa tatizo kubwa la uelewa wa misingi na utawala bora unaozingatia sheria na miiko ya uongozi, tunatoa wito kuwa;
1.Mamlaka yake ya uteuzi, kwa kuchukulia kwa uzito na tahadhari kubwa kauli na mwenendo wa kiuongozi wa Albert Charamila, ichukue hatua dhidi yake ili kujitenga na kauli hizo kwani iwapo zitaachwa bila kukemewa na bila kuchukuliwa hatua, tasfiri moja pekee itakayobakia ni kuwa kauli hizo zinawakilisha msimamo wa Serikali ya CCM na kwamba zina baraka kutoka kwa mamlaka zake za juu.
2.Mamlaka hiyo itambue kuwa ni jambo la hatari kubwa kwa jamii yetu kwa ujumla, husuan kwa mstakabali wa amani na utulivu unaojengwa katika msingi imara wa haki, iwapo watu wenye hulka na silka za kujivunia kupiga, kutesa, kuua watu au kumwaga damu, ndiyo watakuwa wameaminiwa kubeba dhamana za uongozi unaoendana na kufanya maamuzi makubwa kwa niaba ya wananchi. Tunasisitiza ni jambo la hatari na ofisi za umma ambazo ni mali za wananchi zitakuwa zimegeuzwa sawa na vichaka vya kujificha majambazi wanaovaa suti na kusikilizwa wakijisifia kumwaga damu na kuua.
3.Katiba ya Nchi yetu imeweka misingi ya utawala bora unaozingatia sheria na haki za binadamu, hakuna mtu yeyote, wa ngazi yeyote, kwenye nafasi yeyote iwe serikalini au katika jamii, mwenye mamlaka ya kuagiza watu wapigwe, wateswe au wauawe.
Kwa kuzingatia misingi hiyo, vyombo vinavyohusika vichukue hatua dhidi ya Albert Charamila, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, haraka iwezekanavyo kabla hulka na silka zake hazijasababisha maafa makubwa yatakayopelekea majuto kwa wananchi.
4.Vyombo vinavyohusika na ulinzi na usalama, vimchunguze Albert Charamila kwa kauli yake mwenyewe, ambapo amesikika na kuonekana katika hizo video fupi zinazosambaa mitandaoni akijifisia na kujipongeza kwa ama kupiga mtu, kutesa mtu au kuua mtu, kisha akaenda kujipongeza kwa kunywa pombe.
Hitimisho
Pamoja na Chama chake, kupitia mtendaji wake mkuu, kusikika zaidi ya mara moja, kwa kauli nyepesi nyepesi, kikijaribu kujikosha kuwa Albert Charamila hayuko sahihi, mwenendo wake kiuongozi na uthubutu wake wa kuendelea kutoa kauli zinazotishia haki za binadamu na uhai wa watu, bila kukemewa, kukaripiwa au kuadhibiwa na mamlaka za juu yake, zinaibua maswali mengi na kuacha shaka kubwa kuhusu uimara wa Serikali hii kupambana na ukiukwaji mkubwa haki za binadamu, misingi ya demokrasia na utawala bora unaoendelea sehemu zingine nchini.
“Tunajiuliza, iwapo Mkuu wa Mkoa anaweza kutumia nafasi yake, kutoa kauli za kushabikia uhalifu wa kupiga watu, kutesa watu, kuua watu au kumwaga damu, mchana kweupe mbele ya kamera za waandishi wa habari, na hatua zisichukuliwe dhidi yake, je viongozi wenye nafasi hizo au chini yao au juu zaidi, wanatoa maagizo gani au wanajisifia kufanya nini wanapokuwa gizani au sirini au nyuma ya kuta nne kwenye ofisi zetu ambako hakuna kamera?
Ni hatari kubwa kwa kauli hizo kuachwa bila kukemewa, kukaripiwa au serikali kujitenga nazo kwa kuchukua hatua, hasa zinapotolewa katika kipindi hiki ambapo vyombo vinavyohusika na Serikali kwa ujumla haijawahi kuwapatia Watanzania sababu na suluhisho rasmi kutokana na sintofahamu iliyopo ya matukio ya baadhi ya watu kupotea, kuteswa na miili ya watu waliokufa kuokotwa huku vyanzo vya vifo hivyo vikiwa havijulikani.
Imetolewa leo, Ijumaa, Agosti 30, 2019 na;
Tumaini Makene
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano
CHADEMA
Tags