Changamoto za Utalii nchini kutatuliwa
0
August 17, 2019
Serikali kupitia Wizara ya Maliasili na Utalii imesema itaendelea kupunguza adha mbalimbali zinazowakabili Wadau wa Utalii likiwemo suala la polisi wa usalama barabarani kusimamisha magari yenye watalii mara kwa mara.
Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Maliasili na Utalii, Constantine Kanyasu alipokuwa akizungumza na Wadau wa Utalii nchini katika kongamano la Utalii lililofanyika mkoani Arusha.
Amesema Serikali kwa kushirikiana na wadau wa utalii nchini imejenga vituo vya ukaguzi wa magari vya utalii ili kupunguza usumbufu kwa watalii barabarani.
Amesema vituo hivyo vitashughulikia masuala ya msingi likiwemo suala madereva wenye watalii kupimwa kilevi.
Amesema mbali na kilevi, Vituo hivyo vitashughulikia vitendo vyote ya uhalifu watakavyofanyiwa watalii.
Aidha, Kanyasu amesema lengo la Serikali ni kupunguza kero kwa watalii ili wafikie milioni mbili mwaka 2019.
Akizungumza kwenye kongamano hilo,Kanyasu amesema licha ya kujengwa vituo hivyo vya ukaguzi lakini bado kuna kero ambazo zinafanyiwa kazi lengo likiwa ni kuboresha sekta ya utalii.
Kwa upande wake, Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha, Jonathan Shana amewataka wadau wa utalii kufuata sheria lakini akataka kupewa taarifa za polisi wanaowakwaza.
“Nipigieni simu hata saa nane za usiku kwa askari wanaowaomba rushwa nishughulike nao” Alisisitiza Shana.
Naye Mkuu wa mkoa wa Arusha, Mrisho Gambo amesema lengo la Arusha kuanzisha vituo vya ukaguzi magari ni kupunguza kero.