DC Mtatiro Azuia Nyumba ya Watoto Yatima Kuuzwa


Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro, amemwamuru mnunuzi wa nyumba moja na eneo la makazi kata ya Nakayaya Tunduru Mjini, kwenda mahakamani kutafuta haki badala ya kuwaondoa watoto wanne wadogo walioachiwa nyumba hiyo na mama yao aliyefariki Agosti mwaka huu.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na kitengo cha habari Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Mtatiro amechukua hatua hiyo kulinda haki za watoto hao wanne wa marehemu Mwanahawa Faraji Mwenyemvua ambaye aliugua kwa muda mrefu hadi alipofariki mwezi Agosti 2019.

Imeelezwa kuwa baada ya kifo chake, malori yalianza kumwaga mchanga eneo la nyumba hiyo kutoka kwa mtu anayedaiwa kuwa mnunuzi wa eneo hilo, ambapo pamoja na mambo mengine aliwataka watoto hao kuhama mara moja.

Taarifa zilipomfikia Mkuu wa Wilaya ya Tunduru akaambatana na vyombo vya ulinzi na usalama kuzuru eneo hilo Alhamisi jioni na kuita pande zote zinazohusika; mnunuzi, wauzaji wakuu (kaka na dada za marehemu), watoto wa marehemu, majirani, marafiki na ndugu.

Mtatiro alisikiliza pande zote na kubaini kuwa eneo hilo liliuzwa wakati marehemu akiwa hai ili fedha hizo zitumike kwa matibabu yake, lakini akabaini kuwa marehemu hakuwa ameweka sahihi yake japokuwa ndugu wanasisitiza kuwa wakati mauziano yanafanyika marehemu alikuwa na akili timamu na uwezo wa kuzungumza pamoja na kuandika.

Mtatiro amesema kuwa mchakato wa manunuzi ya eneo hilo una mashaka makubwa na amewataka walionunua wakatafute haki hiyo mahakamani, akisisitiza kuwa yeye atawalinda watoto wa marehemu.

Mtatiro amesitisha uendelezaji wa eneo uliokuwa unafanywa na anayedaiwa kulinunua hadi hapo mnunuzi atakapoenda mahakamani kudai eneo hilo kisheria. Mtatiro amesisitiza kuwa, mchakato wowote wenye mashaka unaweza kuamuliwa na mahakama peke yake na siyo mnunuzi, ndugu wa marehemu au watoto wa marehemu.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad