Musoma. Shida Masaba (55), dereva wa Mkuu wa Mkoa wa Mara amesema mwanaye, Kasobi aliyefariki dunia baada ya kupata ajali akiwa anaendesha gari la mkuu huyo wa mkoa, alitaka kumuomba radhi lakini ilishindikana.
Baada ya ajali hiyo iliyotokea Jumapili iliyopita, Kasobi alikimbizwa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara na muda wote alikuwa akitaka kuitiwa baba yake ili amuombe radhi. Alifariki dunia usiku wa kuamkia Jumatatu bila kufanikisha jambo hilo.
Masaba baada ya kupata taarifa za ajali hiyo naye alipata mshtuko na kulazwa katika hospitali hiyo lakini mwanaye hakujua mpaka umauti ulipomkuta.
Akizungumza na Mwananchi leo nyumbani kwake Kigera manispaa ya Musoma, Shida amesema baada ya ajali kutokea kijana wake alipoteza fahamu kabla ya kukimbizwa hospitali.
“Baada ya kupata fahamu alijitahidi kutuma watu waniite ili nifike hospitali aniombe msamaha bila kujua kuwa na mimi nilikuwa nimelazwa hapo ila tulikuwa wodi tofauti.”
“Gari ilipogonga gema alirushwa na kutokea kwenye kioo cha mbele. Alipopata fahamu alitaka tuonane aniombe radhi kwa kitendo kile huku akisema kuwa kutokana na maumivu aliyokuwa nayo asingeweza kupona," amesema Shida.
Mwananchi