Dkt. Mwakyembe atoa pongezi, ‘Mmeonyesha uzalendo wa hali ya juu’


Waziri wa Habari Sanaa Utamaduni na Michezo, Dkt. Harrison Mwakyembe amevipongeza Vyombo vya Habari nchini kwa kazi kubwa ya kizalendo na weledi wa hali ya juu katika kutangaza Mkutano wa 39 wa Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC) uliomalizika jana Jijini Dar es Salaam.

Ametoa pongezi hizo Jijini Dar es salaam ambapo amesema kuwa uandishi wa habari wa kujenga na kukosoa ambao una lengo la kurekebisha unahitaji kupongezwa kwakua unasaidia jamii na Serikali katika kuleta maendeleo ya haraka kwa Taifa.

“Waandishi wa habari mbali na kuutangaza Mkutano wa 39 wa SADC lakini pia wametumia taaluma yao kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatikana hapa nchini kupitia sekta mbalimbali ikiwemo Uwekezaji katika viwanda, Utalii, Uchukuzi na nyinginezo,”amesema Dkt. Mwakyembe.

Aidha, ameongeza kuwa Uenyekiti wa Tanzania ambao unaendeshwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli umeleta ari na matumaini mapya ambayo yatasaidia nchi wanachama kuondoa vikwazo vingi vya kibiashara na mawasiliano ya karibu baina ya nchi wanachama na kujenga ustawi wa uchumi kwa nchi hizo.

Dkt. Mwakyembe amesema kuwa baada ya lugha adhimu ya Kiswahili kutangazwa rasmi kuwa miongoni mwa lugha nne zinazotumika ndani ya Jumuiya hiyo, amewataka Watanzania kutumia fursa hiyo kutangaza bidhaa za lugha hiyo ikwemo uandishi wa vitabu vya kiada, ufundishaji wa lugha hiyo, kuuza Sanaa zinazotokana na lugha hiyo kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad