RAIS wa Zanzibar, Dkt. Ali Mohamed Shein amezitaka Nchi za Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) kuweka mkazo wa matumizi ya bidhaa zake na wataalamu wake wa ndani katika kutengeneza fursa za ajira na masoko ndani ya ukanda huo ili kukuza sekta za viwanda na biashara ndani ya jumuiya hiyo.
Akizungumza katika hafla ya kufunga Maadhimisho na Maonesho ya Nne ya Wiki ya Viwanda katika Nchi za SADC leo Alhamisi (Agosti 8, 2019) Jijini Dar es Salaam, Rais Shein alisema umefika wakati kwa mataifa hayo kuzalisha bidhaa bora zenye kuweza kuleta ushindani katika masoko ya ndani na nje ya Jumuiya hiyo.
Dkt. Shein alisema Mataifa ya SADC hayana budi kutumia fursa ya maonesho hayo katika kutangaza fursa za ujuzi na ubunifu kwa kuzalisha na kutengeneza mtandao wa imara wa mawasiliano baina ya Nchi hizo na kuweza kuwa na soko la pamoja litakalowawezesha kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi wa Mataifa hayo.
Kwa mujibu wa Dkt. Shein aliongeza kuwa ili kufikia malengo ya uzalishaji wa bidhaa bora za viwandani ni wajibu wa Serikali zote kutengeneza mtandao imara wa miundombonu ikiwemo matumizi ya tekonolojia ya habari na mawasiliano kwa kuunda mikakati ya pamoja ya utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Jumuiya hiyo uliolenga katika kuimarisha sekta ya viwanda ndani ya jumuiya hiyo.
“Hatujakataa mchango wa wataalamu na bidhaa za nje, lakini chako ni chako na mwenzako si chako, hivyo hakikunyima usikasirike, ni wakati wetu sasa kuweka mkazo katika kutegemea wataalamu wetu na teknolojia zetu katika uzalishaji wa bidhaa zetu” alisema Dkt. Shein.
Aliongeza kuwa Nchi za Jumuiya hiyo hazina budi kutumia fursa za Maonesho na midahalo mbalimbali ya wataalamu inayojadiliwa katika Mikutano ya Jumuiya hiyo ili kuweza kubaini changamoto na hatua mbalimbali zinazopaswa kuchukuliwa ili kuiwezesha jumuiya hiyo kupiga hatua kubwa za Maendeleo ikiwemo kutengeneza fursa za ajira kwa wananchi wake.
Akifafanua zaidi Dkt. Shein aliongeza kuwa Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile ya Zanzibar zimekuwa zikichukua hatua mbalimbali katika uboreshaji wa miundombinu ya miradi ya Maendeleo ambayo imekuwa kichocheo kikubwa cha fursa za ajira kwa vijana sambamba na kutengeneza mazingira wezeshi kwa sekta binafsi kushiriki katika uchumi wa viwanda.
Akitolea mfano, Dkt. Shein alitaja baadhi ya miradi hiyo ni pamoja na ujenzi wa mradi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa viwanda vikubwa, vya kati na vidogo ambavyo kwa pamoja vinaifanya Tanzania kuwa kielelezo cha mfano katika Nchi za SADC katika utekelezaji wa Ajenda ya Maendeleo ya Viwanda ndani ya Jumuiya hiyo.
Kwa upande wake, Waziri wa Viwanda na Biashara, Innocent Bashungwa alisema maonesho hayo yamekuwa chachu na kipimo kwa Nchi za SADC kutekeleza ajenda yake ya Viwanda, kwa kuwa makundi mbalimbali ya wazalishaji, wafanyabiashara na watoa huduma wameonesha udhubutu wa kufikia malengo hayo katika Nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Aliongeza kuwa jumla ya washiriki 5352 walishiriki katika midahalo mbalimbali ikiwemo Nchi SADC 14, taasisi za umma 64, viwanda 64, taasisi za kifedha 35, ambazo zote kwa pamoja zilitoa uzoefu na kuweza kuongeza fursa ya masoko na kuweza kuimarisha mitandao ya mawasiliano baina yao.
Naye Waziri wa Habari, Utalii na Malikale wa Zanzibar, Mahmoud Thabit Kombo alisema ili kufikia malengo ya Mpango Mkakati wa Jumuiya hiyo, nchi za SADC hazina budi kutoa na kuweka mkazo wa ushiriki wa sekta binafsi katika ujenzi wa uchumi shirikishi, kwa kuwa ushirikiano baina ya sekta hiyo na serikali utawezesha kutengeneza fursa mbalimbali za kiuchumi katika mataifa hayo.
Naye Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo, Dkt. Stagomena Tax, aliisifu Serikali ya Tanzania kwa kuwa mfano ndani ya Jumuiya hiyo katika eneo la ujenzi wa uchumi wa viwanda, na hivyo kuzitaka nchi nyingine kuiga mfano huo ili kuweza kuleta mtangamano ndani ya Nchi wanachama.
Aliongeza kuwa ili kuweza kujenga uchumi jumuishi kwa wananchi ndani ya jumuiya hiyo, Sekretarieti ya jumuiya hiyo itaelekeza nguvu yake katika kuimarisha miundombinu ya usafiri wa bidhaa zilizopo ndani ya jumuiya hiyo, kwani bila miundombinu ya uhakika hakutoweza kuwa na mazingira wezeshi ya kuwasaidia wananchi ikiwemo kuondoa vikwazo vya kibiashara ndani ya jumuiya hiyo