Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake la CHADEMA (BAWACHA), Halima Mdee, amesema asilimia kubwa ya watu wenye nyadhifa mbalimbali nchini, wamekuwa wakiwatumia wanawake kama chombo cha starehe kwa kile alichokidai wanatumia kauli zenye ishara ya kukebehi wanawake.
Halima Mdee ametoa kauli hiyo katika mkutano wake na wanawake wa chama hicho, jijini Dar es salaam, ambapo amewataka wanawake wenzake kuhakikisha wanailinda hadhi ya mwanamke kwenye jamii.
"Kuna kauli za kebehi za hapa Tanzania dhidi ya wanawake, hakuna kipindi ambacho tumetwezeka kama kipindi hichi, sisi kwa kauli za wakubwa ni kama chombo cha starehe na si watu, nawakumbusha wajibu wenu kurudisha heshima ya mwanamke." amesema Halima Mdee.
"Mimi namuonea huruma sana Mamaangu, huwa anasemaga wakati ananizaa mimi hakupata uchungu sana, akaniambia mwanangu sikujua Mungu aliniepusha na uchungu wakati nakuzaa ila nakutana na uchungu kila siku ya utu uzima wako, nikamwonea huruma kwa sababu kila shida ninayopata mimi yeye anakuwa kwenye mateso makubwa."
Halima kwa sasa ni Mbunge wa Kawe jijini Dar es salaam ambapo alishinda nafasi hiyo wakati wa Uchaguzi Mkuu 2015 akimshinda Kipre Warioba.