India Yatangaza Kulifuta Hadhi Maalum Jimbo la Kashmir

India yatangaza kulifuta hadhi maalum jimbo la Kashmir
India leo imetangaza kuifuta hadhi maalum ya jimbo la Kashmir pamoja na kufanya mabadiliko ya utawala wa jimbo hilo katika moja ya hatua nzito kabisa kuwahi kuchukuliwa katika eneo hilo lenye utawala wa ndani.

Uamuzi huo umetangazwa na Waziri wa Mambo ya Ndani wa India, Amit Shah, wakati maelfu ya wanajeshi wakiwasili kwenye jimbo la Kashmir ambalo linapinga kutawaliwa na India.

Kwa mujibu wa shirika la habari DW, Tamko hilo linafuta ibara ya 370 ya katiba ya India ambayo inatoa ruhusa kwa jimbo la Kashmir kuwa na katiba yake yenyewe pamoja na haki ya kufanya maamuzi kuhusu masuala yote isipokuwa ulinzi, mawasiliano na mambo ya kigeni.

Ibara hiyo katiba ambayo itafutwa inawazuia pia raia wa India walio nje ya jimbo la Kashmir kununua ardhi, kufanya kazi katika serikali za mitaa, kupata nafasi za ufadhili wa masomo zinazotolewa kwa ajili ya jimbo hilo, pamoja na kuishi jimboni humo moja kwa moja.

Wakosoaji wa serikali ya India inayoongozwa na jamii ya walio wengi ya wahindu wameitaja hatua hiyo kuwa jaribio la kulazimisha jimbo la Kashmir kuwa chini ya mamlaka kamili ya India na kuruhusu jamii ya wahindu kuchanganyika na wakaazi wa jimbo hilo ambalo wakaazi wake wengi ni waislamu.

Vyombo vya habari vya India vimeripoti kuwa serikali ya India imeamuru jimbo la Kashmir ligawanywe katika maeneo mawili yenye yenye uongozi tofauti ambayo ni Jammu Kashmir na Ladakh.

Hatua hiyo inakuja wakati baada ya siku kadhaa za kukosekana utulivu na kuwasili kwa vikosi vya jeshi kwenye jimbo la Kashmir pamoja na kukamatwa kwa wanasiasa mashuhuri wa jimbo hilo ikiwemo mawaziri viongozi wa zamani, Mehbooba Mufti na Omar Abdullah.

Kwa miongo kadhaa waasi katika eneo la Kashmir lililo chini ya utawala wa India wameongoza mapambano ya kupinga kuwa chini ya India.

Wakaazi wengi wa jimbo hilo wanaunga mkono madai ya waasi yanayotaka jimbo hilo liunganishwe chini ya utawala wa Pakistan au liwe nchi huru na wamekuwa wakishiriki maandamano kupinga utawala wa India.


Uamuzi huo wa India unatarajiwa kuwa utazusha machafuko na kuzidisha mvutano na Pakistan.

India na Pakistan zinadhibiti maeneo tofauti ya jimbo la Kashmir lakini nchi zote mbili zinadai umiliki kamili wa eneo zima na zimepigana vita mbili kuwania eneo hilo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Pakistan Shah Mahmood Qureshi amekiambia kituo kimoja cha televisheni nchini Pakistan kuwa India imefanya kosa kubwa kwa kuiondolea Kashmir hadhi yake maalum na kwamba Pakistan itaongeza juhudi za kidiplomasia kukabiliana na kile alichokiita matendo yanayokiuka sheria.

Kwenye mji mkuu wa Pakistan, Islamabad maelfu ya wanaharakati wanaounga mkono uhuru wa jimbo la Kashmir wameandamana karibu na ubalozi wa India muda mfupi baada ya India kutangaza uamuzi huo.
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad