Japana leo imeadhimisha miaka sabini na nne ya lile shambulizi la Marekani la bomu la atomiki katika mji wa magharibi wa Hiroshima huku maelfu ya watu wakihudhuria hafla hiyo ya kila mwaka.
Washiriki wakiwemo wahanga wa shambulizi hilo, vizazi vyao na wawakilishi wa kigeni walikaa kimya kwa dakika moja ilipotimu saa mbili na robo kwa saa za Japan.
Huo ndio muda ambao Marekani iliangusha bomu hilo la atomiki la B-29 katika mji huo miaka sabini na nne iliyopita Vita vya Pili vya Dunia vilivyokuwa vinaelekea mwisho wake.
Shambulizi hilo la bomu la nyuklia ambalo halikutarajiwa liliwauwa makumi kwa maelfu ya wakaazi kwa sekunde chache tu na mwishoni mwa mwaka huo watu 140,000 walikuwa wamefariki dunia kutokana na bomu hilo.
Siku tatu baadae Marekani iliangusha bomu jengine la atomiki katika mji wa Nagasaki ulioko kisiwa cha Kyushu. Mnamo Agosti 15 mwaka 1945 majeshi ya Japan yalisalimu amri na kufikisha mwisho vita hivyo.