JPM Akutana na Mabalozi wa Tanzania Nje ya Nchi


Rais Dkt. John Pombe Magufuli akizungumza katika Kikao na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali za nje Ikulu jijini Dar es Salaam

Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wamempongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Pombe Magufuli kwa utekelezaji wa miradi mikubwa ya kimkakati ambayo inajengwa kwa fedha za Watanzania.



Mabalozi hao 43 ambao wapo hapa nchini tangu tarehe 13 Agosti, 2019 wametoa pongezi hizo jana tarehe 22 Agosti, 2019 walipokutana na kuzungumza na Rais Magufuli Ikulu Jijini DSM.



Wametoa pongezi hizo baada ya kutembelea mradi wa ujenzi wa bwawa la Nyerere katika Mto Rufiji, mradi wa ujenzi wa reli ya kati kwa kiwango cha kisasa (standard gauge railway), jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Julius Nyerere, mradi wa ujenzi wa barabara za juu katika makutano ya barabara ya Morogoro na Sam Nujoma (Ubungo Interchange), mradi wa upanuzi wa bandari ya DSM, mradi wa usambazaji wa gesi (Taifa Gas), mradi wa udhibiti wa mawasiliano Tanzania na mradi wa ujenzi wa daraja la Tanzanite (New Selander Bridge) katika bahari ya Hindi.




Rais Magufuli akizungumza katika Kikao na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali za nje Ikulu jijini Dar es Salaam



Kwa upande wa Zanzibar wametembelea mradi wa ujenzi wa jengo la biashara na makazi (shopping mall) eneo la Michenzani, mradi wa ujenzi wa jengo la 3 la abiria katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Sheikh Abeid Amani Karume, mradi wa ujenzi wa nyumba za kisasa wa Fumba Wilaya ya Magharibi, mradi wa ujenzi wa barabara ya Kaskazini – Bububu – Mkokotoni na mradi wa ujenzi wa bandari ya mafuta na gesi katika eneo la Manga Pwani.



Mabalozi hao wameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo pamoja na juhudi nyingine kubwa zinazofanywa na Serikali katika nyanja mbalimbali za huduma za jamii zimeleta heshima kwa nchi na machoni mwa Jumuiya ya Kimataifa, na kwamba zimedhihirisha kufikiwa kwa malengo ya Tanzania kuingia katika uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.




Rais Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Mabalozi wanaoiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali za nje mara baada ya kikao chao Ikulu jijini Dar es Salaam.



Pia wamempongeza kwa kuwa Mwenyekiti SADC kwa kipindi cha mwaka mmoja na wameahidi kuongoza vyema katika mikutano ya Mabalozi wa SADC katika nchi wanazowakilisha kwa kuzingatia mwelekeo ambao Mhe. Rais Magufuli ameutoa katika Mkutano wa 39 wa Wakuu wa Nchi na Serikali wa SADC uliofanyika tarehe 17-18 Agosti, 2019 Jijini DSM.



Akizungumza baada ya kuwasilikiza Mabalozi hao, Rais Magufuli amewapongeza kwa kazi wanazozifanya katika nchi wanazoiwakilisha Tanzania na amewataka waendelee kutekeleza majukumu yao kizalendo na kwa kutanguliza maslahi ya Tanzania.



Pamoja na kueleza kuhusu hali ya uchumi wa nchi, juhudi za kuwapelekea maendeleo Watanzania na juhudi za kujenga uwezo wa kujitegemea, Rais Magufuli amewataka Mabalozi hao kutafuta wawekezaji watakaowekeza katika miradi yenye manufaa hapa nchini.


“Nataka Mabalozi mtuletee miradi ya maendeleo, ifike mahali Balozi ujiulize kwa kuwa kwangu Balozi nimepeleka nini nyumbani? Nimewezesha kujengwa kiwanda? Kujengwa barabara? Kujenga daraja au jengo fulani?” Rais Magufuli.



Rais Magufuli amewasisitiza Mabalozi hao kuhakikisha wanasimamia na kufuatilia kwa karibu masuala wanayoamini yana manufaa kwa nchi ikiwemo uwekezaji na kwamba wasikubali kukwamishwa na viongozi ama wizara yoyote.



“Nataka muwe very aggressive, na ukiona mtu anakukwamisha mimi nipo niandikieni uone kama hatakwama yeye, mimi nataka kuona vitu sio maneno maneno” amesisitiza Rais Magufuli.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad