Kesi ya Freeman Mbowe na Vigogo Wengine CHADEMA Kuendelea kwa Siku 5 Mfululizo


Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu,  Dar es Salaam, imekwama kuendelea na kesi ya uchochezi inayowakabili viongozi wa Chadema, akiwemo Mwenyekiti, Freeman Mbowe kwa sababu Mbunge wa Tarime Vijijini, John Heche amefiwa na kaka yake.

Kesi hiyo ilitakiwa kuendelea kusikilizwa jana pamoja na kutolewa uamuzi kuhusu mabishano ya kuangalia picha za video zinazodaiwa kuonyesha wafuasi na washtakiwa wakiandamana.

Wakili Peter Kibatala akiwakilisha washtakiwa, alidai kuwa aliandika barua mahakamani akiomba ruhusa kwa washtakiwa wawili, Mbowe na Heche, kwamba wamefiwa na kaka zao kwa nyakati tofauti, hivyo wanaweza kukwama kufika mahakamani.

“Mheshimiwa tuliandika barua tukidhani wote wangeshindwa kufika mahakamani, lakini kwa bahati mheshimiwa Mbowe ameweza kufika isipokuwa Heche ndio wanazika leo (jana), tunaomba kuahirisha kesi hadi tarehe nyingine,” alidai.

Wakili wa Serikali Mkuu, Faraja Nchimbi, akijibu alidai hana neno la kuongeza katika maombi hayo, isipokuwa alipendekeza kesi ipangwe kwa tarehe za karibu ili shahidi wa sita amalize ushahidi wake.

“Mheshimiwa, shahidi tunamshikilia kwa wiki mbili sasa, anatakiwa kwenda Nairobi kwenye mafunzo, wenzake wameshaenda, tunaomba tarehe ya karibu na mfululizo ili amalize aweze kusafiri,” alidai Nchimbi.

Hakimu Simba alikubali kuahirisha kesi hiyo na kuamuru isikilizwe mfululizo kuanzia Agosti 15, 16, 19, 21 na 22.

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad