Kesi ya TUNDU Lissu Yakumbana na Mapingamizi


Ijumaa Agosti 23, 2019 aliyekuwa mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu alianza kukumbana na vigingi katika harakati zake za kutetea ubunge wake aliovuliwa, baada ya Serikali ya Tanzania kumuwekea pingamizi la awali kwa hoja nane.

Moja ya hoja za  Serikali dhidi ya maombi ya Lissu ya kibali cha kufungua shauri la kupinga kuvuliwa ubunge iliyotikisa Mahakama Kuu, ni kwamba  maombi hayo hayana msingi na nafuu zinazoombwa haziwezi kutolewa.

Wakili wa Serikali mwandamizi, Abubakar Murisha alisema maombi hayo hayakidhi matakwa ya kisheria.

Lissu amefungua maombi katika mahakama hiyo, chini ya hati ya dharura kupitia kwa kaka yake Alute Mughwai, ambaye amempa mamlaka ya kisheria kufanya hivyo, ikiwa ni hatua ya awali kabisa ya kupigania kurudishiwa ubunge wake.



Katika maombi hayo namba 18 ya mwaka 2019, dhidi ya Spika wa Bunge la Tanzania, Job Ndugai, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Lissu anaomba kibali cha kufungua shauri la maombi maalumu kwa lengo la kupata amri mbalimbali kuhusiana na uamuzi huo wa kuvuliwa ubunge.

Amri hizo kwa mujibu wa hati ya maelezo yake ni pamoja na Mahakama kumwamuru Ndugai awasilishe mahakamani taarifa ya kumvua ubunge aliyoitoa bungeni ili iweze kuipitia na kisha iamuru itenguliwe na kutupiliwa mbali.

Nyingine ni mahakama imwamuru Ndugai ampatie (Lissu) nakala ya taarifa ya kumvua ubunge na itoe amri ya kusitishwa kuapishwa kwa mbunge mteule wa jimbo hilo, Miraji Mtaturu (CCM).

Katika maelezo yake Murisha amesema katika maombi ya namna hiyo kuna mambo sita ya kuzingatia, moja likiwa ni kuambatanisha uamuzi unaolalamikiwa.

“Tunasema maombi haya hayakidhi matakwa ya kisheria kwa kuwa hakuna uamuzi ulioambatanishwa unaolalamikiwa ili mahakama iweze kuupitia, jambo ambalo ni hitaji la lazima,” amesema Murisha.

Wakili Murisha aliwasilisha mahakamani kesi kadhaa zilizoamuriwa na Mahakama Kuu na Mahakama ya Rufani kuthibitisha hoja yake hiyo.

Akijibu hoja hiyo Peter Kibatala,  wakili kiongozi wa Lissu, amesema kuambatanisha uamuzi si hitaji la lazima

kisheria.

“Ukisoma kwa mujibu wa kanuni ya 5 ya mwenendo wa mashauri ya mapitio mahakama  kuhusu uamuzi wa mamlaka za kiserikali, hakuna mahali ambapo panatajwa kuwa ni lazima kuambatanisha uamuzi.”

“Hata waliozitunga hawakuweka hilo kama hitaji la lazima kwa kuwa wakati mwingine uamuzi wa mamlaka za Serikali hufanyika kwa maneno tu na kutekelezwa,” amesema Kibatala na kuwasilisha kesi kadhaa kuunga mkono majibu yake hayo.

Wakili Murisha alisimama tena akisisitiza kuwa hoja yake kwamba lazima kuwepo uamuzi na kwamba hata kesi aliyoirejea wakili Kibatala katika ukurasa wa 16 iko wazi.



Pingamizi nane za Serikali

Maombi hayana maana kwa kutoambatanisha uamuzi wa Spika wa Bunge, Job Ndugai anaoulalamikia (Lissu)
Nafuu anazoziomba haziko kwenye kifungu cha sheria alichokitumia katika maombi yake
Alute Mughwai ambaye amefungua maombi hayo kwa niaba ya Lissu hana haki ya kisheria kufanya hivyo kwa kuwa nguvu ya kisheria anayodai kupewa na Lissu ina kasoro za kisheria.
Hati ya kiapo cha Mughwai kinachounga mkono maombi hayo kina kasoro za kisheria
Maombi ni batili kwa kuunganisha maombi (nafuu) za aina mbili tofauti zenye asili tofauti katika hati moja ya maombi.
Nafuu zinazoombwa si miongoni mwa nafuu zinazotolewa katika Sheria ya marejeo ya maamuzi ya mamlaka za Serikali.
Mwombaji hakutumia njia mbadala kutafuta nafuu anazoziomba kabla ya kwenda mahakamani.
Maombi hayana maana kwa kuungwa mkono na hati ya kiapo ambayo maelezo yake hayajathibitishwa na mwombaji
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad