Kikundi au mtu yeyote atakayekwamisha juhudi za Rais Magufuli kukiona cha moto
0
August 21, 2019
Mkuu wa Wilaya ya Same, Rosemary Senyamule, ameonya kuwa mtu yeyote au kikundi chochote kitakachoibuka kukwamisha juhudi za Rais John Magufuli kuvutia uwekezaji wenye tija kiuchumi katika sekta za madini na viwanda wilayani humo atashughulikiwa ipasavyo kwa mujibu wa sheria za nchi.
Senyamule amesema hayo jana Agosti 20, 20119 wakati akifungua mkutano wa siku moja wa baraza la biashara la wilaya hiyo ambalo lilikutana chini ya maofisa wa Wizara ya Viwanda na Biashara.
“Tunataka Same iwe kimbilio la wawekezaji, kwa kutoa huduma nzuri kwao na niseme wazi kwamba hatutamvumilia mtu atakayekwamisha juhudi hizi zilizoanzishwa na Rais wetu,“amesema Senyamule.
Senyamule amesema majadiliano yaliyofanyika baina ya sekta ya umma na binafsi yameweza kutatua matatizo yanayoikabili sekta ya biashara na kwamba hivi sasa baraza hilo limeanzisha vikosi kazi kwa ajili ya kuanza mchakato wa kuvutia wawekezaji katika sekta za utalii, mazingira na biashara, madini na viwanda, kilimo, mifugo na uvuvi, elimu na afya.
Baraza hilo lilikutana kutekeleza agizo la Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, (Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Watu wenye Ulemavu), Jenista Mhagama, aliyeagiza mabaraza yote nchini kuhuishwa kutokana na utendaji wa mabaraza hayo umekuwa siyo endelevu.
Tags