KITAAOLOJIA: Miluzi mingi ya Fid Q imepoteza jibwa!


Hatimaye, Farid Kubanda maarufu “Fid Q” ameachia ‘Kitaaolojia’,  albamu iliyosubiliwa sana na washabiki wa Bongo Flava nchini kwa kipindi kisichopungua miaka 5. Katika kumbukukumbu ya kuzaliwa kwake mwaka huu, Agosti 13, Fid Q ameachia album hii ikiwa ni zawadi kwa washabiki ambao wamekuwa wakimfuatilia kwa kipindi cha muda mrefu.


Albamu hii ambayo ilisubiriwa sana kama ujio wa Masihi, ilizinduliwa katika viwanja vya Samaki Samaki jijini Dar es Salaam; ambapo watu mbalimbali mashuhuri walihusika katika hafla ya uzinduzi.

Uzinduzi wa “kitaaolojia” ni ishara kuwa, muziki wa Bongo flava hivi sasa unarudi katika enzi zile ambazo wasanii walitambulika sana kwa kutoa kanda/ kanda mseto. Fid Q anaungana na wasanii kama Chin Bees, Navy Kenzo, Diamond Platnumz, Vee Money, na wengine wengi ambao miaka ya hivi karibuni wameachia albamu zao.

Ukiachana na kutoa albamu; pia, wasanii wa Bongo Flava hivi sasa upendelea kutoa “EP” ambazo mara nyingi zinakuwa na nyimbo chache sana: nyimbo 3, 4 mpaka 5.

 Ijapo wasanii wengi wameanza kurudi katika utamaduni wa kuachia album, upande wa tamaduni muziki, vijana wanaoimba “Underground Hip hop” kwao kuachia kanda kila mwaka imekuwa ni “rahisi kama asubuhi ya jumapili”.


Fid ameileta “kitaaolojia” ambayo ina nyimbo 23. Kinachowashtua washabiki wengi ni idadi kubwa ya nyimbo ambazo tayari zimekwisha kupigwa katika redio miaka kadhaa iliyopita. wengi wanahoji hivi Farid amewatendea haki washabiki wake ambao wamesubiri hii project kwa zaidi ya miaka 6?

Image result for KITAAOLOJIA
Orodha ya nyimbo zilizopo kwenye albamu ya KITAAOLOJIA
“Kitaaolojia” ni albamu ambayo inanikumbusha “Detox,” ile project ya nguli wa Hip Hop nchini Marekani, Dr. Dre. Kwa zaidi ya miaka 15, Dre alitangaza ujio wa album yake ya nne “Detox” ambayo baadae mwaka 2015 alitangaza ameachana nayo nakutoa “Compton: The Sound Track.”


Kitaaolojia ni album ya tatu “Ngosha” anaitoa muongo mmoja baada ya kutoa Propaganda mwaka 2009, ukiachana na ile maarufu “Vina Mwanzo, Kati na Mwisho” aliyoitoa mwaka 2003. Si ajabu ukijiuliza katika kipindi chote hicho Fid amekuwa akifanya nini?

Jibu ni rahisi sana; Fid Q amekuwa akiachia “hit” singo tu kwa zaidi ya miaka 10 bila ya kutoa album. Pengine washabiki wa muziki wa kizazi hiki hawapendi album au yawezekana pia wasanii nao hawapendi kutoa album? hakuna anayejua, lakini jibu moja ambalo limezoeleka wakiulizwa swali ni kwanini hawatoi album utasikia “album hailipi”

Ajabu zaidi unaweza kusikia kuna wasanii wamekuwa katika gemu kwa zaidi ya miaka 15 au 20 hawana album na pia hawana hata mawazo ya kutoa albamu.

Bila shaka uzoefu wa soko la kimataifa walio nao wasanii kama Vee Money, Diamond Platinumz, Harmonize, na wakina Aika na Nareel walilazimika kutoa albamu bila kupenda. Diamond na Vee wamesainiwa na lebo kubwa ya usambazaji muziki duniani, Sony Music. Hakuna msanii yeyote aliyepo Sony hana albamu ndiyo maana sote tuliona kwa nyakati tofauti waliweza kuachia albamu zao.



Pia, wasanii wa Bongo Flava wanapotoa albamu zao kumekuwa na malalamiko kutoka kwa washabiki, wengi wao wanalalamika kutokuwepo kwa muunganiko au stori kati ya wimbo mmoja kwenda mwingine katika albamu kama alivyowahi kusema Nikki Wapili msanii kutoka kundi la Weusi; je, shida inakuja wapi au ni ugeni katika utamaduni wa kutoa albamu?

Wasanii wengi wa Bongo flava wanatamani kushilikiana na wenzao katika soko la kimataifa; lakini wengi wanakosa vigezo kwasababu ndogo kama kuwa na “profile” ambayo inamtambulisha kimataifa. Mfano hapa Bongo kuna watu kibao wanasubiri kwa hamu ujio mpya wa Kendrick Lamar lakini, hawasumbuki kuwauliza wasanii wanaowapenda hapa Bongo kama Joh Makini ni lini atatoa albamu, kwasababu wanajua kuwa hawana mpango huo.

Nakumbuka kipindi kile rapa Marshal Mathers aka “Eminem” alipopotea katika gemu kwa kipindi cha zaidi ya miaka 5 alipokuja kuachia albamu yake “Relapse” mwaka 2009 pamoja na ile nyingine “Recovery” 2010 kulikuwa kuna kitu kipya katika nyimbo za Eminem kuanzia uchanaji, midundo pamoja na uandishi. Pia, katika promosheni za nyimbo hizo kulikuwa na ubunifu wa hali ya juu ukilinganisha na utaratibu wasanii wa Bongo Fleva hivi sasa wamejiwekea: “listening party” na ziara kwa vyombo vya habari.


Fid Q, ameitoa albam ya “Kitaaolojia” ili apunguze lawama kwa washabiki wake ambao aliwaahidi kutoa “kitaaolojia” miaka kadhaa iliyopita. Album hii ina nyimbo Kkaribia saba ambazo zimekwisha kusikilizwa na washabiki wake tena miaka karibia mitatu nyuma, je, “Kitaaolojia” itaweza kuitikisa “Propaganda” aliyoitoa 2009?



Nilibahatika kusikiliza albamu zilizotolewa na Chin Bees, Navy Kenzo, Diamond Platnumz pamoja na Vanessa Mdee. Nyimbo nyingi zilizokuwamo katika album zao zilikuwa mpya katika masikio ya washabiki wa Bongo Fleva. Mfano, Chin Beez katika album yake “Ladha” 2018 nyimbo zote alizozitoa hazikuwahi kusikilizwa na washabiki wake, ukija kwa msanii kama Vanessa Mdee kwenye “Money Monday” nyimbo nyingi ambazo washabiki wake walikwisha kuzisikia aliziweka kama “bonus tracks”. Fid anakwama wapi?


Ukisikiliza albamu ambazo wana Hip hop nchini wametoa katika miaka ya karibuni utaona kuna ubunifu mkubwa sana. Msanii kama Nikki Mbishi, Nash MC, One the Incredible na wengine kutoka “tamaduni muziki” wamekuwa wakitoa albamu kali sana ambazo Fid Q binafsi alikiri haipiti siku bila kutia masikioni, kulikuwa na haja kubwa sana kwa Fid kupata mawazo kutoka kwa wadogo zake.

Fid Q ni moja ya wasanii ambaye amekuwa akibadilika kila mara, ndio maana ameweza kudumu sana katika gemu ya Bongo Flava. “Hayupo kama alivyokuwa aimaanishi yupo tofauti” lakini “kitaaolojia” sidhani kama imekata kiu ya miaka kadhaa ambayo washabiki wake wamekuwa wakisubili kama ujio wa “Detox” ya Dr. Dre



Imeandikwa na David Andy
Tags

Post a Comment

0 Comments
* Please Don't Spam Here. All the Comments are Reviewed by Admin.

Top Post Ad

Below Post Ad