Kizaazaa Mti wa Mikosi Dar
0
August 06, 2019
MTI aina ya ‘Terminalia Catappa’, unaodaiwa kuwa wa mikosi, umezua kizaazaa upya baada ya watu mbalimbali kuendelea kuukata katika maeneo yanayowazunguka. Hivi karibuni kulizuka sintofahamu baada ya taarifa kuenea kuwa mti huo una mikosi baina ya watu wanaohusiana na hasa wanandoa, hivyo kuanza kuukata kwa kasi. Uwazi lilizungumza na mtu aliyejitambulisha kwa jina moja la Kibonge, mkazi wa Mwenge – Mlalakuwa jijini Dar es Salaam, ambaye alikutwa akikata miti hiyo nyumbani kwake, akisema amepata taarifa kuwa ina mikosi.
“Nimesikia muda mrefu kuwa hii miti ina mikosi lakini nilipuuzia, ila nimesisitizwa madhara yake na ndugu yangu, ndiyo maana nimeamua kuikata. Acha niikate tu, nitapanda aina nyingine. Siwezi kukaa na miti ambayo haina baraka nyumbani kwangu,” alisema Kibonge. Mti huo humea na kuwa mkubwa huku matawi yake yakitengana kati ya matawi na matawi na kutengeneza kitu kama pingili ambapo sasa watu huikata na kusababisha uharibifu wa mazingira.
Lakini Taasisi ya Utafiti ya Misitu nchini (Tafori) na mnajimu (astrologist), wamelazimika kuitoa hofu jamii kuhusu mti aina hiyo kwa kufafanua baada ya kipande cha video chenye sauti ya mtu anayejiita Mtume Vicent Mkalla wa Kanisa la Victory Faith, kueleza madhara ya mti huo alioubatiza jina la ‘mti mfarakano’ au ‘chonganishi’ kuzua sintofahamu.
Mtu huyo alidai mti huo wenye jina la Kigiriki na Kirumi, likimaanisha sehemu za siri za mwanamume, ni mti unao-oa na kutawala. Alisema mahali popote ambako mti huu umejiotea wenyewe au kupandwa, huleta majanga mbalimbali, ikiwamo wanandoa kugombana mara kwa mara au hata kuachana pia husababisha kifo miongoni mwa wanafamilia hususan kwa kina baba au watoto wa kiume ambao hupata maradhi ya ghafla.
Imedaiwa pia kwamba mti huo ukiwa nyumbani kwako au ofisini huleta ugumu wa kifedha na madeni makubwa. Akizungumza na gazeti hili, mnajimu (astrolojist), Maalim Hassan Yahya Hussein alisema, kinyota hakuna kitu kama hicho.
“Sijawahi kujifunza kwenye mambo ya astrology (unajimu) kwamba mti aina yoyote unaweza kuleta mikosi ama vifo au ofisi kukosa fedha. Hizo ni dhana potofu, watu wapuuze,” alisema kwa kifupi Maalim Hassan.
Katika taarifa ya Tafori, iliyotolewa na mkurugenzi wake, Dk. Revocatus Mushumbusi, alisema miti aina hiyo ising’olewe kwa kisingizio cha imani potofu kwani haina madhara yanayoelezwa na kusambazwa kwenye mitandao ya kijamii. “Kuna aina zaidi ya 100 za miti aina ya Terminalia hapa duniani na yote haina madhara yanayotajwa katika taarifa ambazo si rasmi zinazozunguka katika mitandao ya kijamii.
“Hata hivyo, mti unaolaumiwa na kuhusishwa na imani potofu, umetajwa kwa jina la kisayansi kama Terminalia Catappa ‘mkungu’ japo picha zinazozunguka kwenye mitandao ya kijamii ni za mti unaoitwa kwa jina la kisayansi kama Terminalia Mantaly ‘Panga Uzazi’,” alisema.
Alisema aina zote mbili yaani Mkungu ‘Terminalia Catappa’ na Panga Uzazi ‘Terminalia Mantaly’ inafaa kwa bustani na kuboresha mandhari. “Aina hizi mbili za miti ya Terminalia zina tofauti kubwa, Mkungu ina majani mapana, wakati Panga Uzazi, majani yake ni madogo.
“Pia Terminalia Catappa inazaa matunda makubwa yanayoliwa na wanadamu na sehemu nyingi za Tanzania, mti huu umejulikana kama Mkungu, maana unazaa kungu na haujawahi kujulikana kama mti chonganishi sehemu yoyote duniani,” alisema.
Alisema jina la mti Terminalia Catappa halina uhusiano na sehemu za siri za mwanaume, kwani sehemu ya kwanza ya jina hili, yaani ‘Terminalia’ inatokana na neno la Kilatini ‘Terminus’ linaloleta neno la Kiingereza Terminal, yaani ya mwishoni, cha mwishoni, ikimaanisha kwamba majani yake yamekusanyika mwishoni mwa tawi au kijitawi.
Alisema sehemu ya pili ya jina yaani ‘Catappa’, inatokana na neno Ketapang kwa lugha ya Maleshia (Malay), likimaanisha mti wenye mbegu zinazotumika kutengezea dawa. Alisema mti huo unafaa kwa matumizi mbalimbali kama vile mbao na mbegu zake huliwa na zinatoa mafuta yasiyo na harufu ambayo hutumika kutibu uvimbe tumboni na yakichemshwa na majani yake hutibu magonjwa mengi ya ngozi.
Tags