Idara ya Uhamiaji nchini, imemkamata Jasmin Ngongolo, mkazi wa Dar es Salaam, katika uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere akiwa na stika feki za Visa 2,546 za Tanzania akitokea Afrika ya Kusini.
Taarifa hiyo imetolewa na Kamishina wa Uhamiaji, Usimamizi na Udhibiti wa Mipaka Samwel Mahirane, amesema mtuhumiwa huyo alikamatwa tarehe 2 Agosti, 2019, ambapo alifunga mizigo hiyo kwa ustadi ikiwa na utambulisho juu ya kila boksi kuwa ni stika zinazobandikwa katika vioo vya magari.
Amesema, mtuhumiwa alikutwa na bidhaa nyingine ambazo ni sabuni za kuogea, sabuni za unga za kufulia, 'pampers', hereni, pafyumu na vipodozi vya aina mbalimbali kwa lengo la kuwahadaa maofisa wakati wa upekuzi.
"Tumefanikiwa kumkamata pia na mume wa mtuhumiwa ambaye ni Zakayo Stanslaus na anahusishwa na hujuma hiyo kwa kufika uwanja wa ndege kwa ajili ya kumpokea mtuhumiwa," amesema Kamishina Mahirane.
Kamishina Mahirane amesema wamefanikiwa kuwakamata watuhumiwa hao baada ya kupata taarifa kutoka kwa wasamaria wema na kwamba, baada ya uchunguzi kukamilika watuhumiwa hao watafikishwa mahakamani.